Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Matendo 6

6
Mateso Na Kuenea Kwa Injili
(6:1–9:31)
Saba Wachaguliwa Kuhudumu
1 Basi ikawa katika siku hizo, wakati idadi ya wanafunzi ilipokuwa ikiongezeka sana, palitokea manung’uniko kati ya Wayahudi wa Kiyunani, dhidi ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahaulika katika mgawanyo wa chakula wa kila siku. 2 Wale mitume kumi na wawili wakakusanya wanafunzi wote pamoja wakasema, “Haitakuwa vyema sisi kuacha huduma ya neno la Mungu ili kuhudumu mezani. 3 Kwa hiyo ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, watu wenye sifa njema, waliojawa na Roho wa Mwenyezi Mungu na hekima, ambao tunaweza kuwakabidhi kazi hii, 4 nasi tutatumia muda wetu kuomba na huduma ya neno.”
5 Yale waliyosema yakawapendeza watu wote, nao wakamchagua Stefano (mtu aliyejawa na imani na Roho wa Mwenyezi Mungu) pamoja na Filipo, Prokoro, Nikanori, Timoni, Parmena na Nikolao, mwongofu kutoka Antiokia. 6 Wakawaleta watu hawa mbele ya mitume, nao wakawaombea na kuwawekea mikono juu yao.
7 Neno la Mungu likazidi kuenea. Idadi ya wanafunzi ikazidi kuongezeka sana katika Yerusalemu hata makuhani wengi wakaitii ile imani.
Kukamatwa Kwa Stefano
8 Stefano, akiwa amejaa neema na nguvu za Mungu, alifanya ishara na miujiza mikubwa miongoni mwa watu. 9 Hata hivyo, ukainuka upinzani wa watu wa Sinagogi#6:9 Nyumba ya ibada na mafunzo. la Watu Huru (kama lilivyokuwa linaitwa), la Wayahudi wa Kirene na wa Iskanderia, na wengine kutoka Kilikia na Asia. Watu hawa wakaanza kupingana na Stefano. 10 Lakini hawakuweza kushindana na hekima yake wala huyo Roho ambaye alisema kwake.
11 Ndipo kwa siri wakawashawishi watu fulani waseme, “Tumemsikia Stefano akisema maneno ya kufuru dhidi ya Musa na dhidi ya Mungu.”
Stefano Afikishwa Mbele Ya Baraza
12 Wakawachochea watu, wazee na walimu wa Torati, nao wakamkamata Stefano wakamfikisha mbele ya baraza. 13 Wakaweka mashahidi wa uongo ambao walishuhudia wakisema, “Mtu huyu kamwe haachi kusema dhidi ya mahali hapa patakatifu na dhidi ya Torati. 14 Kwa maana tumemsikia akisema kwamba Isa Al-Nasiri atapaharibu mahali patakatifu na kubadili desturi zote tulizopewa na Musa.”
15 Watu wote waliokuwa wameketi katika baraza wakimkazia macho Stefano, wakaona uso wake unang’aa kama uso wa malaika.

Iliyochaguliwa sasa

Matendo 6: NMM

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia