Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 22

22
Kujua Uthabiti Wa Ibrahimu
1 Baadaye Mungu akamjaribu Ibrahimu. Akamwambia, “Ibrahimu!”
Ibrahimu akajibu, “Mimi hapa.”
2 Kisha Mungu akamwambia, “Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, Isaka umpendaye, uende katika nchi ya Moria. Mtoe huko kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”
3 Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaka mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia. 4Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali. 5 Akawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunakwenda kule. Tutakwenda kuabudu na kisha tutawarudia.”
6 Ibrahimu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaka mwanawe, yeye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja, 7 Isaka akanena akamwambia Ibrahimu baba yake, “Baba yangu!”
Ibrahimu akaitika, “Mimi hapa, mwanangu.”
Isaka akasema, “Moto na kuni zipo, Je, yuko wapi mwana-kondoo kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa?”
8 Ibrahimu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja.
9 Walipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaka mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni. 10 Kisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe. 11 Lakini malaika wa bwana akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Ibrahimu! Ibrahimu!”
Akajibu, “Mimi hapa.”
12 Akamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo lolote. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”
13 Ibrahimu akainua macho yake, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake nyuma yake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe. 14 Ibrahimu akapaita mahali pale Yehova-Yire.#22:14 Yehova-Yire maana yake Bwana atatupa. Mpaka siku ya leo inasemekana, “Katika mlima wa bwana itapatikana.”
15 Basi malaika wa bwana akamwita Ibrahimu kutoka mbinguni mara ya pili, 16 akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema bwana, kwamba kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee, 17 hakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga ulioko pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao, 18 na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”
19 Ndipo Ibrahimu akawarudia watumishi wake, wakaondoka wakaenda wote pamoja mpaka Beer-Sheba. Ibrahimu akaishi huko Beer-Sheba.
Wana Wa Nahori
20 Baada ya muda, Ibrahimu akaambiwa, “Milka pia amepata watoto, amemzalia ndugu yako Nahori wana:
21 Usi mzaliwa wake wa kwanza, Buzi nduguye,
Kemueli (baba wa Aramu),
22 Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.”
23 Bethueli akamzaa Rebeka.
Milka alimzalia Nahori nduguye Ibrahimu hao wana wanane.
24 Suria wake Nahori aliyeitwa Reuma pia alikuwa na wana:
Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 22: NMM

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia