Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 27

27
Yakobo Anaipata Baraka Ya Isaka
1Isaka alipokuwa mzee na macho yake yalipokuwa yamekosa nguvu asiweze kuona tena, akamwita Esau mwanawe mkubwa, akamwambia, “Mwanangu.”
Akajibu, “Mimi hapa.”
2Isaka akasema, “Mimi sasa ni mzee na sijui siku ya kifo changu. 3 Sasa basi, chukua silaha zako, podo na upinde, uende nyikani, ukawinde nyama pori kwa ajili yangu. 4Uniandalie aina ya chakula kitamu nikipendacho uniletee nile, ili niweze kukubariki kabla sijafa.”
5Basi Rebeka alikuwa akisikiliza Isaka alipokuwa akizungumza na mwanawe Esau. Esau alipoondoka kwenda nyikani kuwinda nyama pori na kuleta, 6Rebeka akamwambia Yakobo mwanawe, “Tazama, nimemsikia baba yako akimwambia ndugu yako Esau, 7‘Niletee mawindo, kisha ukaniandalie chakula kitamu nile, ili niweze kukubariki mbele za bwana kabla sijafa.’ 8 Sasa, mwanangu, nisikilize kwa makini na ufanye yale ninayokuambia: 9Nenda sasa katika kundi ukaniletee wana-mbuzi wawili wazuri, ili niandalie chakula kitamu kwa ajili ya baba yako, kama vile anavyopenda. 10Kisha umpelekee baba yako ale, ili apate kukubariki kabla hajafa.”
11 Yakobo akamwambia Rebeka mama yake, “Lakini ndugu yangu Esau ana nywele mwilini, mimi nina ngozi nyororo. 12 Itakuwaje kama baba yangu akinigusa? Itaonekana kwake kama niliyemfanyia ujanja na kuleta laana juu yangu badala ya baraka.”
13Mama yake akamwambia, “Mwanangu, laana na iwe juu yangu. Fanya tu ninalokuambia, nenda ukaniletee hao wana-mbuzi.”
14Kwa hiyo alikwenda akawaleta, akampa mama yake, akaandaa chakula kitamu, kama vile alivyopenda baba yake. 15 Kisha Rebeka akachukua nguo nzuri za Esau mwanawe wa kwanza, alizokuwa nazo nyumbani, akamvika Yakobo mwanawe mdogo. 16Pia akamfunika mikononi na sehemu laini ya shingo kwa ngozi za mbuzi. 17Hatimaye akampa Yakobo hicho chakula kitamu pamoja na mkate aliouoka.
18Akamwendea baba yake akasema, “Baba yangu.”
Akajibu, “Naam, mwanangu, wewe ni nani?”
19 Yakobo akamwambia baba yake, “Mimi ni Esau mzaliwa wako wa kwanza. Nimefanya kama ulivyoniambia. Tafadhali uketi, ule sehemu ya mawindo yangu ili uweze kunibariki.”
20Isaka akamuuliza mwanawe. “Umepataje haraka namna hii, mwanangu?”
Akajibu, “bwana Mwenyezi Mungu wako amenifanikisha.”
21 Kisha Isaka akamwambia Yakobo, “Mwanangu tafadhali sogea karibu nami ili nikupapase, nione kama hakika ndiwe Esau mwanangu, au la.”
22Yakobo akasogea karibu na baba yake Isaka, ambaye alimpapasa na kusema, “Sauti ni ya Yakobo, bali mikono ni ya Esau.” 23 Hakumtambua, kwa sababu mikono yake ilikuwa na nywele kama ya ndugu yake Esau, kwa hiyo akambariki. 24Akamuuliza, “Hivi kweli wewe ni mwanangu Esau?”
Akajibu, “Mimi ndiye.”
25 Kisha akasema, “Mwanangu, niletee sehemu ya mawindo yako nile, ili nipate kukubariki.”
Yakobo akamletea naye akala, akamletea na divai akanywa. 26Kisha Isaka baba yake akamwambia, “Njoo hapa, mwanangu, unibusu.”
27 Kwa hiyo akamwendea akambusu. Isaka aliposikia harufu ya nguo zake, akambariki, akasema,
“Aha, harufu ya mwanangu
ni kama harufu ya shamba
ambalo bwana amelibariki.
28 Mungu na akupe umande kutoka mbinguni
na utajiri wa duniani:
wingi wa nafaka na divai mpya.
29 Mataifa na yakutumikie
na mataifa yakusujudie.
Uwe bwana juu ya ndugu zako,
na wana wa mama yako wakusujudie.
Walaaniwe wale wakulaanio,
nao wale wakubarikio wabarikiwe.”
30 Baada ya Isaka kumaliza kumbariki na baada tu ya Yakobo kuondoka kwa baba yake, ndugu yake Esau akaingia kutoka mawindoni. 31 Naye pia akaandaa chakula kitamu akamletea baba yake. Kisha akamwambia, “Baba yangu, keti ule sehemu ya mawindo yangu, ili upate kunibariki.”
32 Isaka baba yake akamuuliza, “Wewe ni nani?”
Akajibu, “Mimi ni mwanao, mzaliwa wako wa kwanza, Esau.”
33 Isaka akatetemeka kwa nguvu sana, akasema, “Alikuwa nani basi, ambaye aliwinda mawindo akaniletea? Nilikula kabla tu hujaja na nikambariki, naye hakika atabarikiwa!”
34 Esau aliposikia maneno haya ya baba yake, akalia sauti kubwa na ya uchungu, na kumwambia baba yake, “Nibariki mimi, mimi pia, baba yangu!”
35 Lakini akasema, “Ndugu yako amekuja kwa udanganyifu na akachukua baraka yako.”
36 Esau akasema, “Si ndiyo sababu anaitwa Yakobo? Amenidanganya mara hizi mbili: Alichukua haki yangu ya kuzaliwa na sasa amechukua baraka yangu!” Kisha akauliza, “Hukubakiza hata baraka moja kwa ajili yangu?”
37 Isaka akamjibu Esau, “Nimemfanya yeye kuwa bwana juu yako, pia nimewafanya ndugu zako wote kuwa watumishi wake, nimemtegemeza kwa nafaka na divai mpya. Sasa nitaweza kukufanyia nini, mwanangu?”
38 Esau akamwambia baba yake, “Je, baba yangu una baraka moja tu? Unibariki mimi pia, baba yangu!” Kisha Esau akalia kwa sauti kubwa.
39 Baba yake Isaka akamjibu, akamwambia,
“Makao yako yatakuwa
mbali na utajiri wa dunia,
mbali na umande wa mbinguni juu.
40 Utaishi kwa upanga,
nawe utamtumikia ndugu yako,
lakini wakati utakapokuwa umejikomboa,
utatupa nira yake
kutoka shingoni mwako.”
Yakobo Anakimbilia Kwa Labani
41 Esau akawa na kinyongo dhidi ya Yakobo kwa ajili ya baraka ambazo baba yake alikuwa amembariki. Akasema moyoni mwake, “Siku za kuomboleza kwa ajili ya baba yangu zimekaribia, ndipo nitamuua ndugu yangu Yakobo.”
42Rebeka alipokwisha kuambiwa yale aliyoyasema Esau mwanawe mkubwa, alimwita Yakobo mwanawe mdogo, akamwambia, “Ndugu yako Esau anajifariji kwa wazo la kukuua. 43 Sasa basi, mwanangu, fanya nisemalo: Kimbilia haraka kwa Labani ndugu yangu kule Harani. 44Ukae naye kwa muda mpaka ghadhabu ya ndugu yako itulie. 45 Wakati ndugu yako atakapokuwa hana hasira nawe tena na amesahau uliyomtendea, nitakupelekea ujumbe urudi. Kwa nini niwapoteze wote wawili kwa siku moja?”
46 Kisha Rebeka akamwambia Isaka, “Nimechukia kuishi kwa sababu ya hawa wanawake wa Kihiti. Ikiwa Yakobo ataoa mke miongoni mwa wanawake wa nchi hii, wanawake wa Kihiti kama hawa, sitakuwa na faida kuendelea kuishi.”

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 27: NMM

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha