33
Yakobo Akutana Na Esau
1 Yakobo akainua macho akamwona Esau akija na watu wake 400, kwa hiyo akawagawanya watoto kati ya Lea, Raheli na wale watumishi wake wawili wa kike. 2Akawaweka wale watumishi wa kike na watoto wao mbele, Lea na watoto wake wakafuata, Raheli na Yusufu wakaja nyuma. 3 Yeye mwenyewe akatangulia mbele na kusujudu mara saba alipomkaribia ndugu yake.
4Lakini Esau akamkimbilia Yakobo kumlaki na kumkumbatia, akamwangukia shingoni na kumbusu. Nao wakalia. 5 Esau akainua macho akawaona wale wanawake na watoto. Akauliza, “Hawa uliofuatana nao ni nani?”
Yakobo akamjibu, “Ni watoto ambao Mungu amempa mtumishi wako kwa neema.”
6Kisha wale watumishi wa kike na watoto wao wakakaribia na kusujudu. 7Kisha Lea na watoto wake wakaja na kusujudu. Mwisho wa wote wakaja Yusufu na Raheli, nao pia wakasujudu.
8 Esau akauliza, “Una maana gani kuhusu makundi hayo yote niliyokutana nayo?”
Akasema, “Ni ili kupata kibali machoni pako, bwana wangu.”
9 Lakini Esau akamwambia, “Ndugu yangu, tayari nina wingi wa mali. Ulivyo navyo viwe vyako mwenyewe.”
10 Yakobo akasema, “La hasha! Tafadhali, kama nimepata kibali machoni pako, upokee zawadi hii kutoka kwangu. Kwa maana kuuona uso wako, ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa takabali kubwa. 11 Tafadhali ukubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea.
12Ndipo Esau akasema, “Na tuendelee na safari, nitakuwa pamoja nawe.”
13 Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu unajua kwamba watoto ni wachanga na kwamba ni lazima nitunze hawa kondoo wake na ng’ombe wanaonyonyesha. Wakipelekwa kwa haraka hata kama ni kwa siku moja tu, wanyama wote watakufa. 14 Hivyo bwana wangu umtangulie mtumishi wako, wakati mimi nikija polepole kwa mwendo wa makundi yaliyo mbele yangu na mwendo wa watoto, mpaka nifike kwa bwana wangu huko Seiri.”
15 Esau akamwambia, “Basi na niwaache baadhi ya watu wangu pamoja nawe.”
Yakobo akauliza, “Lakini kwa nini ufanye hivyo, niache tu nipate kibali machoni pa bwana wangu.”
16 Hivyo siku hiyo Esau akashika njia akarudi Seiri. 17 Pamoja na hayo, Yakobo akaenda Sukothi,#33:17 Sukothi maana yake Vibanda. mahali alipojijengea makazi kwa ajili yake na mabanda kwa ajili ya mifugo yake. Hii ndiyo sababu sehemu ile inaitwa Sukothi.
18 Baada ya Yakobo kutoka Padan-Aramu, alifika salama katika mji wa Shekemu huko Kanaani na kuweka kambi yake karibu na mji. 19 Akanunua kiwanja kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa bei ya vipande mia vya fedha, ambapo alipiga hema lake. 20Pale akajenga madhabahu na kupaita El-Elohe-Israeli.#33:20 El-Elohe-Israeli maana yake Mungu, Mungu wa Israeli au Mwenye Nguvu ni Mungu wa Israeli.