37
Ndoto Za Yusufu
1 Yakobo akaishi Kanaani katika nchi ambayo baba yake alikuwa ameishi.
2 Zifuatazo ni habari za Yakobo.
Yusufu, kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga makundi ya kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake wa mama wengine, yaani wana wa Bilha na wana wa Zilpa wake za baba yake, naye akawa akimletea baba yake taarifa mbaya kuhusu hao ndugu zake.
3 Basi, Israeli akampenda Yusufu kuliko yeyote miongoni mwa kaka zake, kwani ni mwanawe wa uzeeni, akamshonea joho lililorembwa vizuri sana. 4 Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yusufu kuliko yeyote mwingine miongoni mwao, walimchukia na hawakusema naye neno lolote jema.
5Yusufu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi. 6Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota: 7 Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani, ghafula mganda wangu ukasimama wima, wakati miganda yenu ikiuzunguka na kuuinamia.”
8 Ndugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakaongeza kumchukia zaidi kwa sababu ya ndoto yake pamoja na yale aliyowaambia.
9Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine, wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.”
10 Alipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako na mimi na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe hadi nchi?” 11 Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliweka jambo hilo moyoni.
Yusufu Auzwa Na Ndugu Zake
12 Basi, ndugu zake walikuwa wamekwenda kuchunga makundi ya baba yao karibu na Shekemu, 13 naye Israeli akamwambia Yusufu, “Kama ujuavyo, ndugu zako wanachunga makundi huko karibu na Shekemu. Njoo, nitakutuma kwao.”
Yusufu akajibu, “Vema sana, niko tayari.”
14 Kwa hiyo akamwambia, “Nenda uone kama mambo yote ni salama kwa ndugu zako na makundi, kisha uniletee habari.” Ndipo akamtuma Yusufu kutoka Bonde la Hebroni.
Yusufu alipofika Shekemu, 15mtu mmoja akamkuta akizungukazunguka mashambani na akamuuliza, “Unatafuta nini?”
16Akajibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Unaweza kuniambia wanachunga wapi makundi yao?”
17 Yule mtu akajibu, “Wamehama hapa. Nilisikia wakisema, ‘Twende Dothani.’ ”
Kwa hiyo Yusufu akawafuatilia ndugu zake na kuwakuta karibu na Dothani. 18 Ndugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga shauri baya la kumuua.
19 Wakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja! 20 Njooni sasa, tumuue na kumtupa katika shimo mojawapo na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.”
21 Reubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao akasema, “Tusiutoe uhai wake. 22 Tusimwage damu yoyote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani kwa baba yake.
23 Kwa hiyo Yusufu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililorembwa vizuri alilokuwa amevaa. 24 Kisha wakamchukua wakamtupa katika shimo. Wakati huo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji ndani yake.
25 Walipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri.
26 Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini ikiwa tutamuua ndugu yetu na kuificha damu yake? 27 Njooni, tumuuze kwa hawa Waishmaeli. Tusimguse, kwa kuwa hata hivyo yeye ni ndugu yetu, nyama yetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali.
28 Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yusufu kutoka kwenye lile shimo, na kumuuza kwa shekeli ishirini#37:28 Shekeli 20 ni sawa na gramu 200. za fedha kwa wale Waishmaeli, ambao walimpeleka Misri.
29 Reubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yusufu hayupo, alirarua nguo zake. 30 Akawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?”
31Kisha wakalichukua lile joho la Yusufu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu. 32Wakalichukua lile joho lililorembwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.”
33 Baba yao akalitambua akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yusufu ameraruliwa vipande vipande.”
34 Kisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa nguo ya gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi. 35 Wanawe wote na binti zake wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu mpaka nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia.
36 Wakati ule ule, Wamidiani wakamuuza Yusufu huko Misri kwa Potifa, mmojawapo wa maafisa wa Farao, aliyekuwa mkuu wa ulinzi.