40
Mnyweshaji Na Mwokaji
1Baada ya muda, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri. 2 Farao akawakasirikia hawa maafisa wake wawili, mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, 3 akawaweka chini ya ulinzi katika nyumba ya mkuu wa kikosi cha ulinzi katika gereza lile lile alimofungwa Yusufu. 4 Mkuu wa kikosi cha ulinzi akawakabidhi kwa Yusufu, naye akawahudumia.
Walipokuwa wamekaa chini ya ulinzi kwa muda, 5kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti.
6Yusufu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni. 7Ndipo Yusufu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, akasema, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?”
8 Wakamjibu, “Sisi sote tuliota ndoto, lakini hapakuwa na mtu yeyote wa kuzifasiri.”
Ndipo Yusufu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.”
9Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yusufu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu, 10 nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva. 11Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.”
12 Yusufu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu. 13 Katika siku hizi tatu, Farao atakutoa gerezani na kukuweka tena kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mikononi mwake, kama vile ulivyokuwa unafanya ulipokuwa mnyweshaji wake. 14 Lakini wakati mambo yatakapokuwia mazuri, unikumbuke, unifanyie wema, useme mema juu yangu kwa Farao ili niondoke huku gerezani. 15Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lolote linalostahili niwekwe gerezani.”
16 Yule mwokaji mkuu alipoona kuwa Yusufu amefasiri ikiwa na maana nzuri, akamwambia Yusufu, “Mimi pia niliota ndoto: Kichwani mwangu kulikuwepo vikapu vitatu vya mikate. 17Katika kikapu cha juu kulikuwa na aina zote za vyakula vilivyookwa kwa ajili ya Farao, lakini ndege walikuwa wakivila kutoka kwenye kikapu nilichokuwa nimebeba kichwani.”
18 Yusufu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vikapu vitatu ni siku tatu. 19 Katika siku hizi tatu, Farao atakata kichwa chako na kukutundika juu ya mti. Nao ndege watakula nyama ya mwili wako.”
20Mnamo siku ya tatu, ilikuwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Farao, naye akawaandalia maafisa wake wote karamu. Akawatoa gerezani mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, akawaweka mbele ya maafisa wake: 21 Ndipo akamrudisha mnyweshaji mkuu kwenye nafasi yake, ili aweke kikombe mikononi mwa Farao tena, 22lakini akamwangika yule mwokaji mkuu, sawasawa na jinsi Yusufu alivyowaambia katika tafsiri yake.
23 Pamoja na hayo, mnyweshaji mkuu hakumkumbuka Yusufu, bali alimsahau.