42
Ndugu Za Yusufu Waenda Misri
1 Wakati Yakobo alipofahamu kuwa kuna nafaka huko Misri, akawaambia wanawe, “Mbona mnakaa tu hapa mnatazamana?” 2 Akaendelea kuwaambia, “Nimesikia kuwa huko Misri kuna nafaka. Telemkeni huko mkanunue chakula kwa ajili yetu, ili tuweze kuishi wala tusife.”
3Ndipo wale ndugu kumi wa Yusufu, wakateremka huko Misri kununua nafaka. 4 Lakini Yakobo hakumtuma Benyamini, ndugu yake Yusufu, pamoja na wengine, kwa sababu aliogopa asije akapatwa na madhara. 5 Hivyo wana wa Israeli walikuwa miongoni mwa wale waliokwenda Misri kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa katika nchi ya Kanaani pia.
6 Wakati huo Yusufu alikuwa mtawala wa nchi ya Misri, naye alikuwa ndiye aliwauzia watu wote nafaka. Kwa hiyo wakati ndugu zake Yusufu walipofika, wakamsujudia hadi nyuso zao zikagusa ardhi. 7Mara Yusufu alipowaona ndugu zake, akawatambua, lakini akajifanya mgeni na kuzungumza nao kwa ukali, akiwauliza, “Ninyi mnatoka wapi?”
Wakamjibu, “Tumetoka katika nchi ya Kanaani kuja kununua chakula.”
8Ingawa Yusufu aliwatambua ndugu zake, wao hawakumtambua. 9 Ndipo Yusufu alipokumbuka ndoto zake kuwahusu wao, akawaambia, “Ninyi ni wapelelezi! Mmekuja kuangalia mahali ambapo nchi yetu haina ulinzi.”
10Wakamjibu, “Sivyo bwana wangu. Watumishi wako wamekuja kununua chakula. 11Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Watumishi wako ni watu waaminifu, wala sio wapelelezi.”
12Akawaambia, “La hasha! Mmekuja kuangalia mahali ambapo nchi yetu haina ulinzi.”
13 Lakini wakamjibu, “Watumishi wako walikuwa kumi na wawili, wana wa mtu mmoja ambaye anaishi katika nchi ya Kanaani. Sasa mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu na mwingine alikufa.”
14Yusufu akawaambia, “Ni sawa kabisa kama nilivyowaambia: Ninyi ni wapelelezi! 15 Na hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Hakika kama Farao aishivyo, hamtaondoka mahali hapa mpaka ndugu yenu mdogo aje hapa. 16 Tumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu, wengine mtawekwa gerezani, ili maneno yenu yajaribiwe kuona kama mnasema kweli. La sivyo, hakika kama Farao aishivyo ninyi ni wapelelezi!” 17 Akawaweka wote chini ya ulinzi kwa siku tatu.
18 Siku ya tatu Yusufu akawaambia, “Fanyeni hili nanyi mtaishi, kwa maana namwogopa Mungu: 19Ikiwa ninyi ni watu waaminifu, mmoja wa ndugu zenu na abaki kifungoni, nanyi wengine pelekeni nafaka kwa jamaa yenu wanaoteseka kwa njaa. 20Lakini ni lazima mniletee ndugu yenu mdogo hapa, ili maneno yenu yathibitike na kwamba msife.” Wakakubali kufanya hivyo.
21 Wakaambiana wao kwa wao, “Hakika tunaadhibiwa kwa sababu ya ndugu yetu. Tuliona jinsi alivyohuzunika alipokuwa anatusihi kuponya maisha yake, lakini hatukumsikiliza, hiyo ndiyo sababu dhiki hii imetupata.”
22 Reubeni akawajibu, “Sikuwaambieni msitende dhambi dhidi ya kijana? Lakini hamkunisikiliza! Sasa ni lazima tuadhibiwe kwa ajili ya damu yake.” 23 Hawakujua kuwa Yusufu angewaelewa, kwa sababu alitumia mkalimani.
24 Yusufu akajitenga nao akaanza kulia, kisha akawarudia na kuzungumza nao tena. Akataka Simeoni akamatwe na kufungwa mbele yao.
25 Yusufu akatoa amri ya kujaza magunia yao nafaka na kuweka fedha ya kila mmoja ndani ya gunia lake, kisha wapewe mahitaji ya njiani. Baada ya kufanyiwa hayo yote, 26wakapakiza nafaka juu ya punda zao, wakaondoka.
27 Walipofika mahali pa kulala huko njiani mmoja wao akafungua gunia lake ili amlishe punda wake, akakuta fedha yake kwenye mdomo wa gunia lake. 28 Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Iko ndani ya gunia langu.”
Mioyo yao ikazimia, na kila mmoja akamgeukia mwenzake wakitetemeka, wakaulizana, “Ni nini hiki Mungu alichotufanyia?”
29 Walipofika kwa Yakobo baba yao katika nchi ya Kanaani, wakamweleza mambo yote yaliyowapata. Wakasema, 30 “Huyo mtu ambaye ndiye bwana katika nchi hiyo alisema nasi kwa ukali, akatutendea kana kwamba sisi tulikuwa tunaipeleleza nchi. 31Lakini tulimwambia, ‘Sisi ni watu waaminifu, sio wapelelezi. 32Tulizaliwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja. Mmoja alikufa, na mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu huko Kanaani.’
33“Ndipo huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alipotuambia, ‘Hivi ndivyo nitafahamu kuwa ninyi ni watu waaminifu: Mwacheni mmoja wa ndugu zenu pamoja nami hapa, kisha nendeni mpeleke chakula kwa ajili ya jamaa yenu inayoteseka kwa njaa. 34 Lakini mleteni huyo ndugu yenu mdogo kwangu, ndipo nitajua kuwa ninyi sio wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Kisha nitamrudisha ndugu yenu, nanyi mtaweza kufanya biashara katika nchi hii.’ ”
35Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka kwenye magunia yao, ndani ya gunia la kila mtu kulikuwa na mfuko wa fedha! Wakati wao na baba yao walipoona mifuko ya fedha, wakaogopa. 36 Yakobo baba yao akawaambia, “Ninyi mmenipokonya watoto wangu. Yusufu hayupo na Simeoni hayupo tena na sasa mnataka kumchukua Benyamini. Kila kitu ni kinyume nami!”
37Ndipo Reubeni akamwambia baba yake, “Waweza kuwaua wanangu wote wawili, ikiwa sitamrudisha Benyamini kwako. Mkabidhi Benyamini katika uangalizi wangu, nami nitamrudisha.”
38 Lakini Yakobo akasema, “Mwanangu hatashuka huko pamoja nanyi; ndugu yake amekufa naye ndiye peke yake aliyebaki. Ikiwa atapatwa na madhara katika safari mnayoiendea, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini kwa masikitiko.”