20
Kufufuka Kwa Isa
(Mathayo 28:1-8; Marko 16:1-8; Luka 24:1-12)
1 Alfajiri na mapema siku ya kwanza ya juma, kulipokuwa kungali giza bado, Maria Magdalene alikwenda kaburini na kukuta lile jiwe limeondolewa penye ingilio. 2 Hivyo akaja akikimbia kwa Simoni Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine ambaye Isa alimpenda, na kusema, “Wamemwondoa Bwana Isa kaburini, na hatujui walikomweka!”
3 Petro na yule mwanafunzi mwingine wakaondoka mara kuelekea kaburini. 4Wote wawili walikuwa wanakimbia, lakini yule mwanafunzi mwingine akakimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini. 5 Alipofika, akainama na kuchungulia mle kaburini, akaona vile vitambaa vya kitani mle ndani, lakini hakuingia. 6Ndipo Simoni Petro akaja, akimfuata nyuma akaenda moja kwa moja hadi ndani ya kaburi. Naye akaona vile vitambaa vya ile sanda vikiwa pale chini 7 na kile kitambaa kilichokuwa kichwani mwa Isa. Kitambaa hicho kilikuwa kimekunjwa mahali pa peke yake, mbali na vile vitambaa vya kitani vya ile sanda. 8 Kisha yule mwanafunzi aliyetangulia kufika kaburini naye akaingia ndani, akaona, akaamini. 9 (Kwa kuwa mpaka wakati huo walikuwa bado hawajaelewa kutoka Maandiko kwamba ilikuwa lazima Isa afufuke kutoka kwa wafu).
10Kisha hao wanafunzi wakaondoka wakarudi nyumbani kwao.
Isa Anamtokea Maria Magdalene
(Mathayo 28:9-10; Marko 16:9-11)
11 Lakini Maria Magdalene akasimama nje ya kaburi akilia. Alipokuwa akilia, akainama, kuchungulia mle kaburini, 12 naye akaona malaika wawili wamevaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Isa ulipokuwa umelazwa, mmoja upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni.
13 Wakamuuliza Maria, “Mwanamke, mbona unalia?”
Akawaambia, “Nalia kwa kuwa wamemchukua Bwana wangu na sijui walikomweka.” 14 Baada ya kusema hayo, akageuka, akamwona Isa amesimama, lakini hakumtambua.
15 Isa akamwambia, “Mwanamke, mbona unalia? Unamtafuta nani?”
Maria akidhani ya kuwa aliyekuwa anaongea naye ni mtunza bustani, kwa hiyo akamwambia, “Bwana, kama ni wewe umemchukua, tafadhali nionyeshe ulikomweka, nami nitamchukua.”
16 Isa akamwita, “Maria!”
Ndipo Maria akamgeukia Isa na kusema naye kwa Kiebrania, “Rabboni!” (Maana yake Mwalimu).
17 Isa akamwambia, “Usinishike, kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba.#20:17 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Lakini nenda kwa ndugu zangu ukawaambie, ‘Ninapaa kwenda kwa Baba yangu ambaye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu ambaye ni Mungu wenu.’ ”
18 Kwa hiyo Maria Magdalene akaenda kuwatangazia wanafunzi wa Isa, akisema, “Nimemwona Bwana!” Naye akawaambia kwamba Isa alikuwa amemweleza mambo hayo yote.
Isa Awatokea Wanafunzi Wake
(Mathayo 28:16-20; Marko 16:14-18; Luka 24:36-49)
19Ikawa jioni ya ile siku ya kwanza ya juma, wanafunzi wake walikuwa pamoja, milango ikiwa imefungwa kwa kuwaogopa Wayahudi. Naye Isa aliwatokea, akasimama katikati yao, akasema, “Amani iwe nanyi!” 20 Baada ya kusema haya, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Wanafunzi wake wakafurahi sana walipomwona Bwana Isa.
21 Isa akawaambia tena, “Amani iwe nanyi! Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawatuma ninyi.” 22 Naye alipokwisha kusema haya, akawavuvia, akawaambia, “Pokeeni Roho wa Mwenyezi Mungu. 23 Mkimwondolea mtu yeyote dhambi zake, zitaondolewa, na yeyote msiyemwondolea dhambi zake, hazitaondolewa.”
Isa Anamtokea Tomaso
24 Lakini Tomaso, aliyeitwa Didimasi, yaani Pacha, mmoja wa wale kumi na wawili, hakuwa pamoja nao Isa alipokuja. 25 Hivyo wale wanafunzi wengine wakamwambia, “Tumemwona Bwana Isa.”
Lakini yeye akawaambia, “Nisipoona zile alama za misumari mikononi mwake, na kuweka kidole changu kwenye hizo alama za misumari na mkono wangu ubavuni mwake, sitaamini.”
26 Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwa tena pamoja ndani ya nyumba, naye Tomaso alikuwa pamoja nao. Ndipo Isa akaja milango ikiwa imefungwa na kusimama katikati yao akasema, “Amani iwe nanyi.” 27 Kisha akamwambia Tomaso, “Weka kidole chako hapa na uone mikono yangu, nyoosha mkono wako uguse ubavuni mwangu. Usiwe na shaka, bali uamini tu.”
28 Tomaso akamwambia, “Bwana wangu na Mungu wangu!”
29 Isa akamwambia, “Umeamini kwa kuwa umeniona? Wamebarikiwa wale ambao hawajaona lakini wameamini.”
Kusudi La Kitabu Hiki
30 Isa alifanya miujiza mingine mingi mbele za wanafunzi wake, ambayo haikuandikwa katika kitabu hiki. 31 Lakini haya yameandikwa ili mweze kuamini ya kuwa Isa ndiye Al-Masihi, Mwana wa Mungu,#20:31 Yaani Mwana wa asili moja na Mwenyezi Mungu (Yn 1:1-2), wa kiroho, bali si wa kimwili. na kwa kumwamini mpate uzima katika jina lake.