1 Wakorintho 14:26-33
1 Wakorintho 14:26-33 BHN
Ndugu, tuseme nini, basi? Mnapokutana pamoja, mmoja aimbe wimbo, mwingine atoe mafundisho, mwingine awe na ufunuo kutoka kwa Mungu, mwingine atumie kipaji cha kusema kwa lugha ngeni na mwingine afafanue yanayosemwa. Yote yawe kwa ajili ya kulijenga kanisa. Wakiwapo watu wenye vipaji vya kusema kwa lugha ngeni, waseme wawili au watatu, si zaidi, tena mmojammoja; na aweko mtu wa kufafanua yanayosemwa. Lakini kama hakuna awezaye kufafanua, basi, mwenye kusema lugha ngeni anyamaze mkutanoni, aseme na nafsi yake mwenyewe na Mungu. Kuhusu wale wenye kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu, waseme wawili au watatu, na wengine wayapime maneno yao. Ikiwa mmoja anaposema na mwingine wa wasikilizaji amepata ufunuo kutoka kwa Mungu, basi, yule anayesema anyamaze. Maana nyote mwaweza kutangaza ujumbe wa Mungu, mmoja baada ya mwingine, ili nyote mpate kujifunza na kutiwa moyo. Kipaji cha kutangaza ujumbe wa Mungu ni lazima kitawaliwe na huyo mwenye hicho kipaji. Maana Mungu si Mungu wa fujo, ila wa amani.