Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Mambo ya Nyakati 19

19
Mwonaji Yehu amkaripia Yehoshafati
1Mfalme Yehoshafati wa Yuda alirejea salama katika ikulu yake mjini Yerusalemu. 2Lakini mwonaji Yehu mwana wa Hanani, alikwenda kumlaki mfalme, akamwambia, “Je, unadhani ni vema kuwasaidia waovu na kuwapenda wamchukiao Mwenyezi-Mungu? Mambo uliyofanya yamekuletea ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. 3Walakini, kuna wema fulani ndani yako. Umekwisha ziondoa sanamu zote za Ashera, mungu wa kike, na umejitahidi sana kumtafuta Mungu kwa moyo wote.”
Yehoshafati afanya matengenezo
4Mfalme Yehoshafati alikaa Yerusalemu, lakini hata hivyo, mara kwa mara aliwatembelea watu wa Beer-sheba kusini, mpaka milima ya Efraimu, upande wa kaskazini. Alifanya hivyo ili kuwavutia watu wamrudie Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao. 5Aliteua waamuzi katika miji yote ya Yuda yenye ngome, 6akawaambia, “Muwe waangalifu sana wakati mnapoamua, kwa maana hukumu mtoayo hamwitoi kwa amri ya binadamu, bali kwa amri itokayo kwa Mwenyezi-Mungu, naye yu pamoja nanyi mnapotoa uamuzi. 7Basi, sasa mwogopeni Mwenyezi-Mungu, muwe waangalifu katika kila jambo mtakalotenda kwa sababu Mwenyezi-Mungu wetu hatavumilia upotoshaji wa haki, wala upendeleo wala ulaji rushwa.”
8Mjini Yerusalemu, Yehoshafati aliteua Walawi kadhaa, waamuzi na baadhi ya wakuu wa jamaa za Waisraeli wawe waamuzi wa magomvi yahusuyo uvunjaji wa sheria za Mwenyezi-Mungu, au ugomvi baina ya wakazi wa mji. 9Akawaamuru akisema; “Tekelezeni wajibu wenu mkimwogopa Mwenyezi-Mungu, kwa uaminifu na kwa moyo wote. 10Kila mara ndugu zenu kutoka katika mji wowote ule wanapowaletea shtaka lolote kuhusu uuaji, uvunjaji wa sheria, amri, kanuni au maagizo, washaurini vema ili wasije wakamkosea Mwenyezi-Mungu. Msipofanya hivyo, nyinyi pamoja na ndugu zenu mtapatwa na ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu. Lakini mkiutekeleza wajibu wenu, hamtakuwa na hatia. 11Amaria, kuhani mkuu, ndiye atakayesimamia mambo yote yanayomhusu Mwenyezi-Mungu, naye Zebadia mwana wa Ishmaeli, gavana wa Yuda atasimamia mambo yote ya utawala, na Walawi watakuwa maofisa. Jipeni moyo muyatekeleze masharti haya, naye Mwenyezi-Mungu awe pamoja nao walio wema.”

Iliyochaguliwa sasa

2 Mambo ya Nyakati 19: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia