Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Wakorintho 9:1-9

2 Wakorintho 9:1-9 BHN

Si lazima kuandika zaidi kuhusu huduma yenu hiyo kwa ajili ya watu wa Mungu. Ninajua jinsi mlivyo na moyo wa kusaidia, na nilijivuna juu yenu kuhusu jambo hilo mbele ya watu wa Makedonia. Niliwaambia: “Ndugu zetu wa Akaya wako tayari tangu mwaka jana.” Hivyo, moto wenu umekwisha wahimiza watu wengi zaidi. Basi, nimewatuma ndugu zetu hao, ili fahari yetu juu yenu ionekane kwamba si maneno matupu, na kwamba mko tayari kabisa na msaada wenu kama nilivyosema. Isije ikawa kwamba watu wa Makedonia watakapokuja pamoja nami tukawakuta hamko tayari, hapo sisi tutaaibika – bila kutaja aibu mtakayopata nyinyi wenyewe – kwa sababu tutakuwa tumewatumainia kupita kiasi. Kwa hiyo, nimeona ni lazima kuwaomba hawa ndugu watutangulie kuja kwenu, wapate kuweka tayari zawadi yenu kubwa mliyoahidi; nayo ioneshe kweli kwamba ni zawadi iliyotolewa kwa hiari na si kwa kulazimishwa. Kumbukeni: “Apandaye kidogo huvuna kidogo; apandaye kwa wingi huvuna kwa wingi.” Kila mmoja, basi, na atoe kadiri alivyoamua, kwa moyo na wala si kwa huzuni au kwa kulazimishwa, maana Mungu humpenda yule mwenye kutoa kwa furaha. Mungu anaweza kuwapeni nyinyi zaidi ya yale mnayoyahitaji, mpate daima kuwa na kila kitu mnachohitaji, na hivyo mzidi kusaidia katika kila kazi njema. Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Yeye hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini; wema wake wadumu milele.”