Matendo 3:1-10
Matendo 3:1-10 BHN
Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wakienda hekaluni, wakati wa sala. Wakati huo watu walikuwa wanambeba mtu mmoja kiwete tangu kuzaliwa. Watu hao walikuwa wakimweka huyo mtu kila siku kwenye mlango wa hekalu uitwao “Mlango Mzuri,” ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia hekaluni. Alipowaona Petro na Yohane wakiingia hekaluni, aliwaomba wampe chochote. Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, “Tutazame!” Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao. Kisha Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu, lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!” Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu. Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu. Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu. Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule “Mlango Mzuri” wa hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata.