Kumbukumbu la Sheria 28:58-68
Kumbukumbu la Sheria 28:58-68 BHN
“Kama msipokuwa waangalifu kutekeleza maneno yote ya sheria hii iliyoandikwa katika kitabu hiki na msipoliheshimu na kulitukuza jina tukufu la kuogofya la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, basi, Mwenyezi-Mungu atawaleteeni nyinyi na wazawa wenu mateso yasiyo ya kawaida, mateso makali yasiyoponyeka na ya kudumu, na magonjwa makali ya kudumu. Atawaleteeni tena yale magonjwa mliyoyaogopa nchini Misri, nayo yatawaandama daima. Atawaleteeni magonjwa ya kila aina na mateso mengine ambayo hayakutajwa katika kitabu hiki cha sheria mpaka muangamie. Ijapokuwa nyinyi ni wengi kama nyota za mbinguni, lakini mtakuwa wachache tu kwa kuwa hamkutii sauti ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Kama vile Mwenyezi-Mungu alivyopendezwa kuwafanikisha na kuwafanya kuwa wengi, vivyo hivyo Mwenyezi-Mungu atapendezwa kuwaletea maafa na kuwaangamiza. Nanyi mtaondolewa katika nchi hiyo ambayo mnakwenda kuimiliki. Mwenyezi-Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka pembe moja ya dunia hadi nyingine na huko mtaitumikia miungu mingine ya miti na mawe, miungu ambayo nyinyi wala wazee wenu hawakuijua. Hamtakuwa na raha yoyote mahali penu wenyewe pa kutulia wala miongoni mwa mataifa hayo. Ila Mwenyezi-Mungu atawapeni huko wasiwasi wa moyo, kufifia kwa macho na mahangaiko ya rohoni. “Maisha yenu yatakuwa mashakani, mchana na usiku mtakuwa na hofu na hamtakuwa na usalama wa maisha. Mioyo yenu itajaa woga wa kila mtakachoona. Asubuhi mtasema, ‘Laiti ingekuwa jioni,’ jioni itakapofika mtasema, ‘Laiti ingekuwa asubuhi.’ Mwenyezi-Mungu atawarudisheni Misri kwa meli, safari ambayo aliahidi kwamba hamngeifanya tena. Huko mtajaribu kujiuza kwa maadui zenu kuwa watumwa, lakini hakuna mtu atakayewanunua.”