Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Kutoka 8:1-15

Kutoka 8:1-15 BHN

Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie Mwenyezi-Mungu asema hivi: Waache watu wangu waondoke ili wanitumikie. Lakini ukikataa kuwaacha waondoke, basi, nitaipiga nchi yako yote kwa kuiletea vyura. Mto Nili utafurika vyura, nao wataingia mpaka ndani ya nyumba yako, chumba chako cha kulala, kitandani mwako, na katika nyumba za watumishi wako na watu wako. Vyura hao wataingia katika majiko yenu na vyombo vyenu vya kukandia unga. Vyura watapanda juu ya mwili wako, miili ya watu wako na watumishi wenu!” Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Mwambie Aroni anyoshe mkono wake na fimbo yake juu ya mito, juu ya mifereji na madimbwi, nao vyura watatokea na kuenea kila mahali nchini Misri.” Basi, Aroni akanyosha fimbo yake juu ya maji yote, vyura wakatokea na kuifunika nchi nzima ya Misri. Lakini wachawi wa Misri kwa uchawi wao pia wakaleta vyura nchini Misri. Kisha Farao akamwita Mose na Aroni, akamwambia, “Msihi Mwenyezi-Mungu, ili aniondolee mimi na watu wangu vyura hawa, nami nitawaacha Waisraeli waende zao na kumtambikia Mwenyezi-Mungu.” Mose akamjibu Farao, “Haya! Waweza kutaja wakati unaotaka nikuombee kwa Mungu, niwaombee maofisa wako na watu wako; nitamwomba awaangamize vyura hawa waliomo katika nyumba zenu; watabaki tu mtoni Nili!” Farao akamwambia, “Kesho.” Mose akasema, “Nitafanya kama unavyosema, ili ujue kwamba hakuna yeyote anayelingana na Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu. Vyura wataondoka kwako, na kwenye nyumba zenu, kwa maofisa wako na kwa watu wako; watabaki tu katika mto Nili.” Basi, Mose na Aroni wakaondoka nyumbani kwa Farao, na Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu amwondolee Farao uvamizi wa vyura hao aliomletea. Mwenyezi-Mungu akafanya kama Mose alivyomwomba: Vyura wakafa majumbani, viwanjani na kwenye kumbi za nyumba na katika mashamba. Watu wakawakusanya vyura hao marundo marundo; nchi nzima ikanuka. Lakini Farao alipoona kwamba nchi imepata nafuu, akawa mkaidi tena, wala hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama Mwenyezi-Mungu alivyokuwa amesema.

Soma Kutoka 8