Ezekieli 17:1-21
Ezekieli 17:1-21 BHN
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu! Tega kitendawili, uwaambie fumbo Waisraeli. Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kulikuwa na tai mmoja mkubwa sana aliyekuwa na mabawa makubwa, yenye manyoya marefu mengi yenye rangi za kila aina. Tai huyo aliruka mpaka mlimani Lebanoni, akatua juu ya kilele cha mwerezi; akakwanyua tawi lake la juu zaidi, akalipeleka katika nchi ya wafanyabiashara, akaliweka katika mji wao mmoja. Kisha akachukua mmea mchanga nchini Israeli, akaupanda katika ardhi yenye rutuba ambako kulikuwa na maji mengi. Mmea ukakua ukawa mzabibu wa aina ya mti utambaao; matawi yake yakamwelekea, na mizizi yake ikatanda chini yake. Mzabibu ukachipua matawi na majani mengi. Lakini kulikuwa na tai mwingine mkubwa; alikuwa na mabawa makubwa ya manyoya mengi. Basi, ule mzabibu ukamtandia mizizi yake, ukamwelekezea matawi yake, ili aumwagilie maji. Mzabibu ulikuwa umetolewa kitaluni mwake ukapandikizwa penye udongo mzuri na maji mengi, ili upate kutoa matawi na kuzaa matunda uweze kuwa mzabibu mzuri sana! Sasa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuuliza: Je, mzabibu huo utaweza kustawi? Je, hawatangoa mizizi yake na kuozesha matunda yake na matawi yake machanga kuyanyausha? Hakutahitajika mtu mwenye nguvu au jeshi kuungoa kutoka humo ardhini. Umepandikizwa, lakini, je, utastawi? Upepo wa mashariki uvumapo juu yake utanyauka; utanyauka papo hapo kwenye kuta ulikoota.” Kisha neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: “Sasa waulize hao watu waasi kama wanaelewa maana ya mfano huo. Waambie kuwa, mfalme wa Babuloni alikuja Yerusalemu, akamwondoa mfalme na viongozi wake, akawapeleka Babuloni. Kisha akamtawaza mmoja wa jamaa ya kifalme, akafanya naye mapatano, akamwapisha. Aliwaondoa humo nchini watu mashujaa akawapeleka mbali ili utawala huo uwe dhaifu na uzingatie agano lake mfalme wa Babuloni. Lakini yule mfalme mpya alimwasi mfalme wa Babuloni kwa kuwatuma wajumbe Misri kuomba farasi na askari wengi. Je, mfalme huyo atafaulu? Je, anayefanya hivyo na kuvunja agano lake ataweza kuepa adhabu? “Mimi Mwenyezi-Mungu naapa kwamba, kama niishivyo, mfalme huyu atafia katika nchi ya Babuloni, nchi ya mfalme yule aliyemweka awe mfalme, na ambaye amedharau kile kiapo na kuvunja lile agano alilofanya naye. Hakika, Farao pamoja na jeshi lake kubwa hataweza kumsaidia vitani wakati Wababuloni watakapomzungushia ngome na kuta ili kuwaua watu wengi. Kwa kuwa alikidharau kile kiapo na kuvunja lile agano ambalo aliahidi kwa mkono wake mwenyewe na kufanya mambo haya yote, hakika hataokoka. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema, kama niishivyo, kwa vile amekidharau kiapo alichoapa kwa jina langu na agano langu akalivunja, hakika nitamwadhibu vikali. Nitatandaza wavu wangu juu yake, naye atanaswa katika mtego wangu; nitampeleka mpaka Babuloni na kumhukumu kwa sababu ya uhaini alioufanya dhidi yangu. Majeshi yake hodari yatauawa kwa upanga na watakaosalia hai watatawanyika pande zote. Hapo mtatambua kuwa mimi, naam, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”