Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 17

17
Mfano wa tai na mzabibu
1Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: 2“Wewe mtu! Tega kitendawili, uwaambie fumbo Waisraeli. 3Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Kulikuwa na tai mmoja mkubwa sana
aliyekuwa na mabawa makubwa,
yenye manyoya marefu mengi
yenye rangi za kila aina.
Tai huyo aliruka mpaka mlimani Lebanoni,
akatua juu ya kilele cha mwerezi;
4akakwanyua tawi lake la juu zaidi,
akalipeleka katika nchi ya wafanyabiashara,
akaliweka katika mji wao mmoja.
5Kisha akachukua mmea mchanga nchini Israeli,
akaupanda katika ardhi yenye rutuba
ambako kulikuwa na maji mengi.
6Mmea ukakua ukawa mzabibu
wa aina ya mti utambaao;
matawi yake yakamwelekea,
na mizizi yake ikatanda chini yake.
Mzabibu ukachipua matawi na majani mengi.
7Lakini kulikuwa na tai mwingine mkubwa;
alikuwa na mabawa makubwa ya manyoya mengi.
Basi, ule mzabibu ukamtandia mizizi yake,
ukamwelekezea matawi yake,
ili aumwagilie maji.
8Mzabibu ulikuwa umetolewa kitaluni mwake
ukapandikizwa penye udongo mzuri na maji mengi,
ili upate kutoa matawi na kuzaa matunda
uweze kuwa mzabibu mzuri sana!
9Sasa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nakuuliza:
Je, mzabibu huo utaweza kustawi?
Je, hawatangoa mizizi yake
na kuozesha matunda yake
na matawi yake machanga kuyanyausha?
Hakutahitajika mtu mwenye nguvu au jeshi
kuungoa kutoka humo ardhini.
10Umepandikizwa, lakini, je, utastawi?
Upepo wa mashariki uvumapo juu yake utanyauka;
utanyauka papo hapo kwenye kuta ulikoota.”
Maelezo yake
11Kisha neno la Mwenyezi-Mungu likanijia: 12# 17:12-15 Taz 2Fal 24:15-20; 2Nya 36:10:13 “Sasa waulize hao watu waasi kama wanaelewa maana ya mfano huo. Waambie kuwa, mfalme wa Babuloni alikuja Yerusalemu, akamwondoa mfalme na viongozi wake, akawapeleka Babuloni. 13Kisha akamtawaza mmoja wa jamaa ya kifalme, akafanya naye mapatano, akamwapisha. Aliwaondoa humo nchini watu mashujaa akawapeleka mbali 14ili utawala huo uwe dhaifu na uzingatie agano lake mfalme wa Babuloni. 15Lakini yule mfalme mpya alimwasi mfalme wa Babuloni kwa kuwatuma wajumbe Misri kuomba farasi na askari wengi. Je, mfalme huyo atafaulu? Je, anayefanya hivyo na kuvunja agano lake ataweza kuepa adhabu?
16“Mimi Mwenyezi-Mungu naapa kwamba, kama niishivyo, mfalme huyu atafia katika nchi ya Babuloni, nchi ya mfalme yule aliyemweka awe mfalme, na ambaye amedharau kile kiapo na kuvunja lile agano alilofanya naye. 17Hakika, Farao pamoja na jeshi lake kubwa hataweza kumsaidia vitani wakati Wababuloni watakapomzungushia ngome na kuta ili kuwaua watu wengi. 18Kwa kuwa alikidharau kile kiapo na kuvunja lile agano ambalo aliahidi kwa mkono wake mwenyewe na kufanya mambo haya yote, hakika hataokoka.
19“Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema, kama niishivyo, kwa vile amekidharau kiapo alichoapa kwa jina langu na agano langu akalivunja, hakika nitamwadhibu vikali. 20Nitatandaza wavu wangu juu yake, naye atanaswa katika mtego wangu; nitampeleka mpaka Babuloni na kumhukumu kwa sababu ya uhaini alioufanya dhidi yangu. 21Majeshi yake hodari yatauawa kwa upanga na watakaosalia hai watatawanyika pande zote. Hapo mtatambua kuwa mimi, naam, mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Ahadi ya Mungu ya tumaini
22Bwana Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi mwenyewe nitachukua kisehemu cha ncha ya juu ya mwerezi, naam, nitavunja tawi changa kutoka matawi yake ya juu na kulipanda juu ya mlima mrefu sana. 23Naam, nitalipanda juu ya mlima mrefu wa Israeli ili lichanue na kuzaa matunda. Litakuwa mwerezi mzuri, na ndege wa aina zote watakaa chini yake pia watajenga viota vyao katika matawi yake.#17:23 Kigiriki: Lakini maneno na wanyama wa kila aina watakaa chini yake. 24Ndipo miti yote nchini itajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu huiporomosha miti mirefu na kuikuza miti mifupi. Mimi hukausha miti mibichi na kustawisha miti mikavu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema hayo na nitayafanya.”

Iliyochaguliwa sasa

Ezekieli 17: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia