Ezekieli 18:21-32
Ezekieli 18:21-32 BHN
“Kama mtu mwovu akiachana na dhambi zake zote alizotenda, kama akishika kanuni zangu zote, akatenda yaliyo ya haki na sawa, huyo hakika ataishi, hatakufa. Makosa yake yote aliyofanya hayatakumbukwa; kwa sababu ya uadilifu wake ataishi. Je, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nafurahia kufa kwake mtu mwovu? La hasha! Mimi napendelea aachane na njia zake mbaya apate kuishi. “Lakini, mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake, akatenda uovu na kufanya machukizo yaleyale anayofanya mtu mwovu, je, huyo ataishi? La! Matendo yake yote mema aliyotenda hayatakumbukwa tena; atakufa kwa sababu ya uasi na dhambi aliyotenda. “Lakini nyinyi mwasema, ‘Hicho afanyacho Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Sikilizeni sasa, enyi Waisraeli: Je, ninachofanya mimi si sawa? Mnachofanya nyinyi ndicho kisicho sawa. Mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake na kutenda uovu atakufa kwa ajili hiyo; atakufa kwa sababu ya uovu aliotenda. Lakini mtu mwovu akiachana na uovu aliofanya, akatenda mambo yaliyo haki na sawa, huyo atayaokoa maisha yake. Kwa kuwa amefikiri, akaachana na makosa aliyoyafanya, hakika ataishi; hatakufa. Lakini nyinyi Waisraeli mwasema, ‘Anachotenda Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Enyi Waisraeli, je, ninachofanya mimi si sawa? Mnachofanya nyinyi ndicho kisicho sawa. “Kwa hiyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nasema hivi: Nitawahukumu nyinyi Waisraeli, kila mmoja wenu, kulingana na mwenendo wake. Tubuni na kuachana na makosa yenu, yasije yakawaangamiza. Tupilieni mbali dhambi mlizonitendea; jipatieni moyo na roho mpya. Enyi Waisraeli, ya nini mfe? Sifurahii kifo cha mtu yeyote. Hivyo tubuni ili mpate kuishi. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”