Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 19:1-14

Ezekieli 19:1-14 BHN

Mungu aliniambia niimbe utenzi huu wa maombolezo kuhusu wakuu wa Israeli: Mama yenu alikuwa simba wa fahari miongoni mwa simba wengine. Alikaa kati ya simba vijana, akawalisha watoto wake. Alimlea mtoto mmojawapo wa watoto wake, mtoto huyo naye akawa simba kijana hodari. Akajifunza kwa mama yake kuwinda, akawa simba mla watu. Mataifa yakapiga mbiu ya hatari dhidi yake, wakamnasa katika mtego wao, wakampeleka kwa ndoana mpaka Misri. Mama yake alipoona kuwa amechoka kungoja, matumaini ya kumpata yamekwisha, alimchukua mtoto wake mwingine, akamfanya simba kijana hodari. Huyo alipokuwa amekua, akaanza kuzurura na simba wengine. Naye pia akajifunza kuwinda, akawa simba mla watu. Aliziandama ngome za watu na kuiharibu miji yao. Nchi ikatishika pamoja na wakazi wake, kwa sauti ya kunguruma kwake. Mataifa yakamkabili kutoka mkoani mwao kote, wakatandaza wavu wao juu yake, naye akanaswa katika mtego wao. Kwa ndoana wakamtia katika kizimba chao, wakampeleka kwa mfalme wa Babuloni. Huko, wakamtia gerezani, ili ngurumo yake isisikike tena juu ya milima ya Israeli. Mama yako alikuwa kama mzabibu shambani, uliopandikizwa kando ya maji, ambao ulizaa sana kwa kuwa na maji tele. Ulikuwa na matawi yenye nguvu, ambayo yalikuwa fimbo za kifalme. Mzabibu huo ulikua kupita miti mingine, watu waliusifu ukubwa wa shina lake na wingi wa matawi yake. Lakini ulingolewa kwa hasira ukatupwa chini ardhini; upepo wa mashariki ukaukausha, matunda yake yakapukutika; matawi yake yenye nguvu yalikaushwa, nao moto ukauteketeza. Na sasa umepandikizwa jangwani, katika nchi kame isiyo na maji. Lakini moto umetoka kwenye shina lake, umeyateketeza matawi na matunda yake. Matawi yake kamwe hayatakuwa na nguvu, wala hayatakuwa fimbo za kifalme. Huo umekuwa wimbo wa maombolezo; ndivyo unavyoimbwa daima.