Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Ezekieli 20:18-32

Ezekieli 20:18-32 BHN

“Niliwaonya wazawa wao kule jangwani: ‘Msizifuate desturi za wazee wenu, msishike amri zao wala msijitie unajisi kwa kuziabudu sanamu za miungu yao. Mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu. Fuateni kanuni zangu, shikeni amri zangu kwa uangalifu. Fanyeni Sabato zangu kuwa takatifu, ili ziwe ishara ya agano langu nanyi. Hizo zitawakumbusha kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ni Mungu wenu.’ “Lakini hata wazawa wao hao waliniasi. Hawakufuata kanuni zangu, hawakushika wala kutekeleza amri zangu ambazo mtu akizishika, huishi. Walizikufuru Sabato zangu. Basi nikasema kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuitimiza hasira yangu juu yao huko jangwani. Lakini nilizuia mkono wangu kwa sababu ya heshima ya jina langu ili nisidharauliwe kati ya watu wa mataifa walioona nikiwatoa nchini Misri. Hata hivyo, niliapa hukohuko jangwani kuwa ningewapeleka katika nchi za mbali na kuwafanya waishi miongoni mwa mataifa ya kigeni, kwa sababu hawakufuata amri zangu, bali walizikataa kanuni zangu, wakazikufuru Sabato zangu na kuziabudu sanamu za miungu ya wazee wao. “Tena niliwapa kanuni mbaya na amri ambazo mtu akizifuata hataishi. Nikawaacha watiwe unajisi kwa tambiko zao za kuwatoa wazaliwa wao wa kwanza kafara kwa sanamu za miungu. Hili lilikuwa pigo lao la adhabu ya kutisha ili watambue kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu. “Sasa, wewe mtu, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Wazee wenu walinikufuru kila mara kwa kukosa uaminifu. Maana nilipowapeleka katika ile nchi niliyoapa kuwapa, kila walipoona kilima kirefu au miti ya majani mengi, walianza kutoa matambiko na tambiko zao na kunichokoza. Hukohuko walitoa tambiko za harufu nzuri na kumimina tambiko za kinywaji. (Mimi nikawauliza, ‘Mahali hapo palipoinuka mnapokwenda panaitwaje?’ Wao wakapaita ‘Mahali palipoinuka’ mpaka leo.) Basi, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawauliza hivi: Je, mtajitia unajisi kwa kufuata desturi za wazee wenu na kuviabudu vitu vinavyonichukiza? Mnapoendelea kutoa tambiko zenu na kuwapitisha watoto wenu motoni mnajitia unajisi mpaka leo hii. Je, nitaulizwa shauri nanyi, enyi watu wa Israeli? Lakini, kama niishivyo, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu naapa kwamba sitakubali kuulizwa shauri nanyi. Nyinyi mnasema mioyoni mwenu, ‘Tutakuwa kama mataifa mengine, kama makabila ya nchi nyingine na kuabudu miti na mawe.’ Hayo mnayopania mioyoni mwenu hayatafanikiwa kamwe.