Ezekieli 22:1-16
Ezekieli 22:1-16 BHN
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Ewe mtu! Uko tayari kutoa hukumu, kuuhukumu mji huu wa wauaji? Basi, ujulishe machukizo yake yote. Uambie, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Wewe ni mji unaowaua watu wako mwenyewe na kujitia unajisi kwa kufanya sanamu za miungu; kwa hiyo wakati wako wa adhabu umewadia. Una hatia kutokana na damu uliyomwaga. Umejifanya najisi kwa sanamu ulizojifanyia. Siku yako ya adhabu umeileta karibu nawe; naam, siku zako zimehesabiwa. Ndio maana nimekufanya udhihakiwe na mataifa na kudharauliwa na nchi zote. Nchi zote za mbali na karibu zitakudhihaki. Umejipatia sifa mbaya na kujaa fujo. “Wakuu wa Israeli walioko kwako, kila mmoja kadiri ya nguvu zake huua watu. Kwako baba na mama wanadharauliwa. Mgeni anayekaa kwako anapokonywa mali yake. Yatima na wajane wanaonewa. Wewe umedharau vyombo vyangu vitakatifu na kuzikufuru sabato zangu. Kwako wamo wanaowasingizia wengine ili wauawe. Wakazi wako hushiriki chakula kilichotolewa kwa miungu milimani. Watu wako wanatenda ufisadi. Kwako wamo watu ambao hulala na wake za baba zao. Huwanajisi wanawake katika siku zao za hedhi. Wengine hufanya machukizo kwa kulala na wake za majirani zao. Wengine hulala na wake za watoto wao, na wengine hulala na dada zao. Huko kwako kuna watu ambao huua kwa malipo. Umepokea riba na kuwalangua wenzako ili kujitajirisha, na kunisahau mimi kabisa! Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. “Nimekunja ngumi yangu dhidi yako kwa sababu ya hiyo faida uliyopata kwa njia isiyo halali na kwa mauaji yaliyofanyika kwako. Je, utaweza kustahimili kuwa hodari siku nitakapopambana nawe? Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema na nitayatekeleza hayo. Nitakutawanya kati ya mataifa na kukutupatupa katika nchi nyingine. Nitaukomesha uchafu ulioko kwako. Utajiweka najisi mbele ya mataifa mengine, lakini utatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”