Mwanzo 14:17-24
Mwanzo 14:17-24 BHN
Abramu aliporudi baada ya kumshinda mfalme Kedorlaomeri na wenzake, mfalme wa Sodoma alitoka kwenda kumlaki katika bonde la Shawe, (yaani Bonde la Mfalme). Naye Melkisedeki, mfalme wa mji wa Salemu, ambaye alikuwa kuhani wa Mungu Mkuu, akaleta mkate na divai, akambariki Abramu akisema, “Abramu na abarikiwe na Mungu Mkuu, Muumba mbingu na dunia! Na atukuzwe Mungu Mkuu, aliyewatia adui zako mikononi mwako!” Naye Abramu akampa Melkisedeki mchango wake sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, “Nipe hao watu, lakini jichukulie mali yote wewe mwenyewe.” Lakini Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu, aliyeumba mbingu na dunia, kwamba sitachukua uzi au kamba ya kiatu, wala chochote kilicho chako, usije ukajivuna na kusema kwamba umenitajirisha. Basi, sitachukua chochote isipokuwa tu vile vitu vijana wangu walivyokula na sehemu ya wale waliokuwa pamoja nami, Aneri, Eshkoli na Mamre ambao wana haki nayo.”