Hosea 14:4-9
Hosea 14:4-9 BHN
Mwenyezi-Mungu asema, “Nitaponya utovu wao wa uaminifu; nitawapenda tena kwa hiari yangu, maana sitawakasirikia tena. Nitakuwa kama umande kwa Waisraeli nao watachanua kama yungiyungi, watakuwa na mizizi kama mwerezi wa Lebanoni. Chipukizi zao zitatanda na kuenea, uzuri wao utakuwa kama mizeituni, harufu yao nzuri kama maua ya Lebanoni. Watarudi na kuishi chini ya ulinzi wangu, watastawi kama bustani nzuri. Watachanua kama mzabibu, harufu yao nzuri kama ya divai ya Lebanoni. Enyi watu wa Efraimu, mna haja gani tena na sanamu? Mimi ndiye ninayesikiliza sala zenu, mimi ndiye ninayewatunzeni. Mimi nitawapa kivuli kama mberoshi, kutoka kwangu mtapata matunda yenu. Yeyote aliye na hekima ayaelewe mambo haya, mtu aliye na busara ayatambue. Maana njia za Mwenyezi-Mungu ni nyofu; watu wanyofu huzifuata, lakini wakosefu hujikwaa humo.”