Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Hosea 4:10-19

Hosea 4:10-19 BHN

Watakula, lakini hawatashiba; watazini, lakini hawatapata watoto, kwa sababu wameniacha mimi Mwenyezi-Mungu, na kufuata miungu mingine. “Divai mpya na ya zamani huondoa maarifa. Watu wangu huomba shauri kutoka kwa mti; kijiti chao cha ramli ndicho kinachowapa kauli. Nia ya kufanya uzinzi imewapotosha; wamefanya uzinzi kwa kufuata miungu mingine, wakaniacha mimi Mungu wao. Wanatambikia kwenye vilele vya milima; naam, wanatoa tambiko vilimani, chini ya mialoni, migude na mikwaju, maana kivuli chao ni kizuri. “Kwa hiyo binti zenu hufanya uzinzi, na bibiarusi wenu hufanya uasherati. Lakini sitawaadhibu binti zenu wanapofanya uzinzi, wala bibi arusi wenu wanapofanya uasherati, maana, wanaume wenyewe ndio wanaofuatana na wazinzi, na kutambikia pamoja nao katika ibada za uzinzi. Watu hawa watovu wa akili hakika wataangamia! “Ama kweli nyinyi Waisraeli ni wazinzi! Lakini, msiwafanye watu wa Yuda wawe na hatia! Msiende mahali patakatifu huko Gilgali, wala msiende kule Beth-aveni. Wala msiape mkisema, ‘Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo!’” Waisraeli ni wakaidi kama punda. Kwa nini basi Mungu ashughulike kuwachunga, kama kondoo kwenye malisho mapana? “Watu wa Efraimu wamejifunga na sanamu. Haya! Waache waendelee tu! Kama vile genge la walevi, wanajitosa wenyewe katika uzinzi; wanapendelea aibu kuliko heshima yao. Basi, kimbunga kitawapeperusha, na watayaonea aibu matambiko yao kwa miungu ya uongo.

Soma Hosea 4