Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Yeremia 15

15
Hukumu kwa watu wa Yuda
1Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia: “Hata kama Mose na Samueli wangesimama mbele yangu na kunisihi, nisingewahurumia watu hawa. Waondoe kabisa mbele yangu. Waache waende zao! 2Na wakikuuliza, ‘Twende wapi?’ wewe utawajibu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi:
Waliopangiwa kufa kwa maradhi, watakufa kwa maradhi;
waliopangiwa kufa kwa upanga, watakufa kwa upanga;
waliopangiwa kufa kwa njaa, watakufa kwa njaa;
na waliopangiwa kuwa mateka, watatekwa mateka.
3Mimi Mwenyezi-Mungu nimeamua kuwaletea aina nne za maangamizi: Vita itakayowaua, mbwa watakaowararua; ndege wa angani watakaowadonoa na wanyama wa porini watakaowatafuna na kuwamaliza. 4Nitawafanya kuwa kitu cha kutisha kwa falme zote za dunia, kwa sababu ya mambo ambayo Manase mwana wa Hezekia, aliyafanya huko Yerusalemu, alipokuwa mfalme wa Yuda.
5“Ni nani atakayewahurumia, enyi watu wa Yerusalemu?
Ni nani atakayeomboleza juu yenu?
Nani atasimama kuuliza habari zenu?
6Nyinyi mmenikataa mimi, nasema mimi Mwenyezi-Mungu;
nyinyi mmeniacha mkarudi nyuma.
Hivyo nimenyosha mkono kuwaangamiza,
kwa kuwa nimechoka kuwahurumia.
7Nimewapepeta kwa chombo cha kupuria,
katika kila mji nchini;
nimewaangamiza watu wangu,
kwa kuwaulia mbali watoto wao,
lakini hawakuacha njia zao.
8Wajane wao wamekuwa wengi
kuliko mchanga wa bahari.
Kina mama wa watoto walio vijana
nimewaletea mwangamizi mchana.
Nimesababisha uchungu na vitisho
viwapate kwa ghafla.
9Mama aliyesifika kuwa na watoto saba;
sasa ghafla hana kitu.
Ametoa pumzi yake ya mwisho,
jua lake limetua kukiwa bado mchana;
ameaibishwa na kufedheheshwa.
Na wale waliobaki hai nitawaacha
wauawe kwa upanga na maadui zao.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”
Yeremia anamlalamikia Mungu
10Ole wangu, mama yangu, kwamba ulinizaa! Mimi nimekuwa mtu wa ubishi na ugomvi nchini pote! Sijapata kukopesha mtu wala kukopeshwa na mtu, lakini kila mtu ananiapiza. 11Haya basi, ee Mwenyezi-Mungu, acha laana hizo nizipate kama sijakutumikia vema na kama sikukusihi kwa ajili ya maadui zangu wakati walipokuwa katika taabu na shida! 12Je, mtu aweza kuvunja chuma, chuma kitokacho kaskazini, au shaba?
13Mwenyezi-Mungu asema: “Nitaifanya mali yenu na hazina zenu zichukuliwe nyara tena bila kulipwa fidia yoyote kwa sababu ya dhambi zenu zote mlizotenda kila mahali nchini. 14Nitawafanya muwatumikie maadui zenu katika nchi msiyoijua kwa sababu hasira yangu imewaka moto ambao hautazimwa milele.”
15Nami nikasema: “Lakini wewe Mwenyezi-Mungu wajua;
unikumbuke na kuja kunisaidia.
Nilipizie kisasi watesi wangu.
Wewe u mvumilivu, usiniache niangamie;
kumbuka kuwa ninatukanwa kwa ajili yako.
16Mara maneno yako yalipofika, niliyameza;
nayo yakanifanya niwe na furaha,
yakawa utamu moyoni mwangu,
maana mimi najulikana kwa jina lako,
ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi.
17Sikuketi pamoja na wanaostarehe,
wala sikufurahi pamoja nao.
Niliketi peke yangu nimelemewa nguvu yako;
kwa maana ulinijaza hasira yako.
18Kwa nini mateso yangu hayaishi?
Mbona jeraha langu haliponi,
wala halitaki kutibiwa?
Ama kweli umenidanganya,
kama kijito cha maji ya kukaukakauka!”
19Mwenyezi-Mungu akajibu:
“Kama ukinirudia nitakurudishia hali ya kwanza,
nawe utanitumikia tena.
Kama ukisema maneno ya maana na sio ya upuuzi,
basi utakuwa msemaji wangu.
Watu watakuja kujumuika nawe,
wala sio wewe utakayekwenda kwao.
20Mbele ya watu hawa,
nitakufanya ukuta imara wa shaba.
Watapigana nawe,
lakini hawataweza kukushinda,
maana, mimi niko pamoja nawe,
kukuokoa na kukukomboa.
Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.
21Nitakuokoa mikononi mwa watu waovu,
na kukukomboa makuchani mwa wakatili.”

Iliyochaguliwa sasa

Yeremia 15: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia