Mathayo 9:1-17
Mathayo 9:1-17 BHN
Yesu alipanda mashua, akavuka ziwa na kufika katika mji wake. Hapo watu walimletea mtu mmoja aliyepooza mwili, amelazwa juu ya kitanda. Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Jipe moyo mwanangu! Umesamehewa dhambi zako.” Baadhi ya waalimu wa sheria wakaanza kufikiri, “Mtu huyu anamkufuru Mungu!” Yesu aliyajua mawazo yao, akasema, “Kwa nini mnawaza mabaya mioyoni mwenu? Ni lipi lililo rahisi zaidi: Kusema, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Simama, utembee?’ Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo duniani wa kuwasamehe watu dhambi.” Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, “Inuka, chukua kitanda chako, uende nyumbani kwako.” Huyo mtu aliyekuwa amepooza akainuka, akaenda nyumbani kwake. Watu wote katika ule umati walipoona hayo, walishangaa na kuogopa; wakamtukuza Mungu aliyewapa binadamu uwezo wa namna hiyo. Yesu aliondoka hapo, na alipokuwa anakwenda zake, alimwona mtu mmoja aitwaye Mathayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Basi, Yesu akamwambia, “Nifuate.” Naye Mathayo akainuka, akamfuata. Yesu alipokuwa nyumbani ameketi kula chakula, watozaushuru wengi na wahalifu walikuja wakaketi pamoja naye na wanafunzi wake. Mafarisayo walipoona hayo, wakawaambia wanafunzi wake, “Mbona mwalimu wenu anakula pamoja na watozaushuru na wenye dhambi?” Yesu aliwasikia, akasema, “Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Basi, kajifunzeni maana ya maneno haya: ‘Nataka huruma, wala si tambiko.’ Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi.” Kisha wanafunzi wa Yohane Mbatizaji walimwendea Yesu, wakamwuliza, “Sisi na Mafarisayo hufunga mara nyingi; mbona wanafunzi wako hawafungi?” Yesu akawajibu, “Je, walioalikwa harusini hutakiwa kuomboleza wakati bwana arusi yupo pamoja nao? La, hasha! Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga. “Watu hawatii kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu. Maana kiraka hicho kitararua hilo vazi kuukuu, na pale palipokuwa pameraruka pataongezeka. Wala watu hawaweki divai mpya katika viriba vikuukuu. Wakifanya hivyo, viriba hupasuka na divai ikamwagika, navyo viriba vikaharibika. Ila, watu huweka divai mpya katika viriba vipya, na vyote viwili, viriba na divai, vikahifadhiwa salama.”