Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mika 3

3
Mika anawashutumu viongozi wa Israeli
1Sasa sikilizeni enyi wakuu wa wazawa wa Yakobo,
sikilizeni, enyi watawala wa wazawa wa Israeli!
Nyinyi ndio mnaopaswa kujua mambo ya haki.
2Lakini nyinyi mnachukia mema na kupenda maovu.
Mnawachuna ngozi watu wangu,
na kubambua nyama mifupani mwao.
3Mnajilisha kwa nyama ya watu wangu
mnawachuna ngozi yao,
mnaivunjavunja mifupa yao,
na kuwakatakata kama nyama ya kupika,
kama nyama ya kutia ndani ya chungu.
4Wakati unakuja ambapo mtamlilia Mwenyezi-Mungu,
lakini yeye hatawajibu.
Atauficha uso wake wakati huo,
kwa sababu mmetenda mambo maovu.
5Mwenyezi-Mungu asema hivi
kuhusu manabii wanaowapotosha watu wake;
manabii ambao hutabiri amani wakipewa kitu,
lakini huwatishia watu kwa vita wasipopewa kitu:
6“Kwenu manabii kutakuwa usiku bila maono,
kutakuwa giza kwenu bila ufunuo.
Kwenu manabii kutakuchwa,
mchana utakuwa giza kwenu.”
7Mabingwa wa maono watafedheheka,
mafundi wa kubashiri wataaibishwa;
wote watafunga midomo yao,
maana hawatapata jibu lolote kutoka kwa Mungu.
8Lakini kwa upande wangu,
nimejazwa nguvu na roho ya Mwenyezi-Mungu;
nimejaliwa kujua haki na kuwa na uwezo
niwatangazie wazawa wa Yakobo kosa lao,
niwaambie Waisraeli dhambi yao.
9Sikieni jambo hili enyi viongozi wa wazawa wa Yakobo,
sikilizeni, enyi watawala wa Waisraeli:
Nyinyi mnachukia mambo ya haki
na kupotosha mambo ya adili.
10Nyinyi mnajenga mji wa Siyoni kwa damu,
naam, mji wa Yerusalemu kwa dhuluma.
11Waamuzi hufanya kazi yao kwa rushwa,
makuhani wake hufundisha kwa malipo,
manabii hutabiri kwa fedha.
Hata hivyo hujidai kumtegemea Mwenyezi-Mungu,
wakisema, “Mwenyezi-Mungu, si yupo pamoja nasi?
Hatutapatwa na madhara yoyote!”
12Haya! Kwa sababu yenu,
Siyoni utalimwa kama shamba,
Yerusalemu utakuwa magofu,
nao mlima wa hekalu utakuwa msitu.

Iliyochaguliwa sasa

Mika 3: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia