Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mika 5

5
Kiongozi mpya kutoka Bethlehemu
1Jumuikeni mkajikusanye enyi watu wa Yerusalemu;
mkisema: “Tumezingirwa, tumesongwa;
naye kiongozi wa Israeli wanampiga shavuni kwa fimbo.”
2Mwenyezi-Mungu asema,
“Lakini wewe Bethlehemu katika Efratha,
wewe ni mdogo tu kati ya jamii za Yuda,
lakini kwako kutatoka mtawala
atakayetawala juu ya Israeli kwa niaba yangu.
Asili yake ni ya zama za kale.”
3Hivyo Mungu atawaacha watu wake kwa maadui,
mpaka yule mama mjamzito atakapojifungua.
Kisha ndugu zake waliobakia,
watarudi na kuungana na Waisraeli wenzao.
4Huyo mtawala atawachunga watu wake kwa nguvu ya Mwenyezi-Mungu,
kwa fahari yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.
Watu wake wataishi kwa usalama,
maana atakuwa mkuu mpaka miisho ya dunia.
5Yeye ndiye atakayeleta amani.
Ukombozi na adhabu
Waashuru wakivamia nchi yetu,
na kuupenya ulinzi wetu,
tutapeleka walinzi wawakabili,
naam, tutawapeleka viongozi wetu kwa wingi.
6Kwa silaha zao wataitawala nchi ya Ashuru,
na kuimiliki nchi ya Nimrodi.#5:5 kadiri ya Mwanzo 10:8-11 Nimrodi alikuwa babu wa watu walioishi huko Mesopotamia.
Watatuokoa mikononi mwa Waashuru,
watakapowasili mipakani mwa nchi yetu
na kuanza kuivamia nchi yetu.
7Wazawa wa Yakobo watakaobaki hai
wameenea miongoni mwa mataifa mengi,
watakuwa kama umande wa Mwenyezi-Mungu uburudishao,
kama manyunyu yaangukayo penye nyasi
ambayo hayasababishwi na mtu
wala kumtegemea binadamu.
8Wazawa wa Yakobo watakaobaki hai,
wameenea miongoni mwa mataifa na watu wengi
watakuwa na nguvu kubwa
kama simba kati ya wanyama wa porini,
kama mwanasimba miongoni mwa makundi ya kondoo,
ambaye kila mahali apitapo,
huyarukia na kuyararua mawindo yake,
asiwepo mtu yeyote wa kuyaokoa.
9Waisraeli watawashinda adui zao
na kuwaangamiza kabisa.
10Mwenyezi-Mungu asema,
“Wakati huo nitawaondoa farasi wenu,
na kuyaharibu magari yenu ya farasi.
11Nitaiharibu miji ya nchi yenu,
na kuzibomolea mbali ngome zenu.
12Nitatokomeza matendo yenu ya uchawi,
nanyi hamtakuwa tena na wapiga ramli.
13Nitaziharibu sanamu zenu,
na nguzo zenu za ibada;
nanyi mtakoma kuabudu vitu mlivyotengeneza wenyewe.
14Nitazing'oa sanamu za Ashera kutoka kwenu,
na kuiangamiza miji yenu.
15Kwa hasira na ghadhabu yangu,
nitalipiza kisasi mataifa yote yasiyonitii.”

Iliyochaguliwa sasa

Mika 5: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia