Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Marko 6:30-44

Marko 6:30-44 BHN

Wale mitume walirudi, wakakusanyika mbele ya Yesu, wakamwarifu yote waliyotenda na kufundisha. Yesu akawaambia, “Twendeni peke yetu mpaka mahali pa faragha mkapumzike kidogo.” Alisema hivyo kwa kuwa kulikuwa na watu wengi mno waliokuwa wanafika hapo na kuondoka hata Yesu na wanafunzi wake hawakuweza kupata nafasi ya kula chakula. Basi, wakaondoka peke yao kwa mashua, wakaenda mahali pa faragha. Lakini watu wengi waliwaona wakienda, wakawatambua. Hivyo wengi wakatoka katika kila mji, wakakimbilia huko Yesu na wanafunzi wake walikokuwa wanakwenda, wakawatangulia kufika. Aliposhuka pwani, Yesu aliona umati mkubwa wa watu, akawaonea huruma, kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Akaanza kuwafundisha mambo mengi. Saa za mchana zilikwisha pita. Basi, wanafunzi wakamwendea Yesu, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, na sasa kunakuchwa. Afadhali uwaage watu waende mashambani na katika vijiji vya jirani, wanunue chakula.” Lakini Yesu akawaambia, “Wapeni nyinyi chakula.” Nao wakamwuliza, “Je, twende kununua mikate kwa fedha dinari 200, na kuwapa chakula?” Yesu akawauliza, “Mnayo mikate mingapi? Nendeni kutazama.” Walipokwisha tazama, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.” Basi, Yesu akawaamuru wanafunzi wawaketishe watu wote makundimakundi penye nyasi. Nao wakaketi makundimakundi ya watu 100 na ya watu hamsini. Kisha Yesu akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akavibariki, akaimega mikate, akawapa wanafunzi wake wawagawie watu. Na wale samaki wawili pia akawagawia wote. Watu wote wakala, wakashiba. Wakaokota mabaki ya mikate na samaki pia, wakajaza vikapu kumi na viwili. Nao waliokula hiyo mikate walikuwa wanaume 5,000.