Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi 9

9
Shukrani kwa Mungu
(Kwa Mwimbishaji: Mtindo wa Muth-labeni. Zaburi ya Daudi)
1Nitakushukuru Mungu kwa moyo wangu wote;
nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu.
2Nitafurahi na kushangilia kwa sababu yako;
nitaliimbia sifa jina lako, ewe Mungu Mkuu.
3Wakati ulipotokea, maadui zangu walirudi nyuma,
walijikwaa na kuangamia.
4Umenitetea kuhusu kisa changu cha haki;
umeketi katika kiti chako cha enzi,
ukatoa hukumu iliyo sawa.
5Umeyakemea mataifa,
umewaangamiza waovu;
majina yao umeyafutilia mbali milele.
6Maadui wameangamia milele;
umeingolea mbali miji yao,
kumbukumbu lao limetoweka.
7Lakini Mwenyezi-Mungu anatawala milele;
ameweka kiti chake cha enzi apate kuhukumu.
8Anauhukumu ulimwengu kwa haki;
anayaamua mataifa kwa unyofu.
9Mwenyezi-Mungu ni ngome ya watu wanaoonewa;
yeye ni ngome nyakati za taabu.
10Wanaokujua wewe, ee Mungu hukutegemea,
wewe Mwenyezi-Mungu huwatupi wakutafutao.
11Mwimbieni sifa Mwenyezi-Mungu akaaye Siyoni.
Yatangazieni mataifa mambo aliyotenda!
12Mungu hulipiza kisasi kwa umwagaji damu;
kamwe hasahau kilio cha wanaoonewa.
13Unirehemu, ee Mwenyezi-Mungu!
Ona mateso ninayoteswa na wanaonichukia;
wewe waninyakua kutoka nguvu za kifo,
14nisimulie sifa zako mbele ya watu wa Siyoni,
nipate kushangilia kwa sababu umeniokoa.
15Watu wa mataifa wametumbukia katika shimo walilochimba,
wamenaswa miguu katika wavu waliouficha.
16Mwenyezi-Mungu amejionesha alivyo;
ametekeleza hukumu.
Watu waovu wamenaswa kwa matendo yao wenyewe.
17Waovu wataishia kuzimu;
naam, mataifa yote yanayomsahau Mungu.
18Lakini fukara hawatasahauliwa daima;
tumaini la maskini halitapotea milele.
19Inuka, ee Mwenyezi-Mungu!
Usimwache binadamu ashinde.
Uyakusanye mataifa mbele yako, uyahukumu.
20Uyatie hofu, ee Mwenyezi-Mungu,
watu wa mataifa watambue kuwa wao ni watu tu!

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi 9: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia