Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zaburi UTANGULIZI

UTANGULIZI
Kitabu cha Zaburi ni kimojawapo cha vitabu vya Biblia katika orodha ya vitabu vya Agano la Kale. Ni kitabu kirefu kuliko vitabu vingine vya Biblia. Kitabu chenyewe ni cha pekee kwa sababu, ingawa kinachukuliwa kama kitabu kimoja, ni mkusanyiko wa namna ya mashairi ya aina na nyakati mbalimbali. Tunabainisha Zaburi ambazo ni nyimbo za kumsifu na kumwabudu Mungu; kuna Zaburi ambazo ni sala za kumwomba Mungu msaada, ulinzi au ukombozi; Zaburi nyingine ni za kumwomba Mungu msamaha, kumshukuru na kumwomba awaadhibu maadui. Zaburi nyingine ni tenzi za mtindo fasaha wa hekima na shabaha yake huwa kufunza ubora wa maisha n.k.
Baadhi ya Zaburi zahusu mahitaji ya mtu binafsi, hali nyingine zahusu taifa zima, aghalabu juu ya mahitaji, mawazo na matazamio ya watu wote wa Mungu. Zaburi zatufundisha jinsi binadamu awezavyo kuzungumza na Mungu. Katika Zaburi, tunakumbana na mambo yanayomshughulisha binadamu, yanayomtatiza na yanayomfurahisha. Ndio maana watu wa Israeli, katika historia yao ndefu, walitia maanani maneno ya Zaburi, wakazitumia kama sala na kuziimba. Hali kadhalika, Yesu na wafuasi wake walizitumia. Vivyo hivyo, tangu mwanzo wa Kanisa, Zaburi zimekuwa kitabu maalumu cha sala kwa Kanisa lote la Kikristo.
Mafungu ya Zaburi
Katika kitabu cha Zaburi kuna vifungu kadha wa kadha ambavyo vimewekwa pamoja kwa sababu fulani maalumu: Nyingine zimewekwa pamoja kwa kuwa zina kichwa kile kile kwa mfano, Zaburi za Asafu (73-83) au za Wakorahi (baadhi zikiwa 42-49). Nyingine zimewekwa pamoja kutokana na matumizi yake, kwa mfano, Zaburi za kuhiji (120-134) au Zaburi za kumsifu Mungu aliye Mfalme au Mtawala wa wote (93-99).
Nyakati za baadaye Zaburi ziligawanywa pia katika vitabu vitano:
Kitabu 1 (1–41)
Kitabu 2 (42–72)
Kitabu 3 (73–89)
Kitabu 4 (90–106)
Kitabu 5 (107–150)
Mgawanyo huo huenda ulifanyika kuiga mgawanyo wa mkusanyiko wa Sheria au “Tora” (Kiebrania) katika vitabu vitano. Kila fungu au kitabu humalizia kwa tamko la sifa kwa Mungu: 41:13; 72:19; 89:52; 106:48; na Zaburi yote ya 150 ambayo ni ya kumsifu Mungu. Zaburi hii ya 150 pia yaonekana kuwa ni tamko la kumsifu Mungu la kumalizia kitabu chote cha Zaburi.
Mashairi ya Kiebrania
Zaburi zina kitu kimoja ambacho chatumika katika Zaburi zote, yaani, mtindo wa kishairi. Jambo hili ni muhimu kwa msomaji aweze kuzielewa inavyotakiwa na mitindo hiyo.
Muundo wa kishairi unaoonekana mara nyingi ni ule wa kupanga mistari ya beti au aya, kwa kawaida mistari miwili hata zaidi ifanane kimaana. Shabaha yenyewe ikiwa au kusisitiza kwa kusema namna nyingine kilichosemwa katika mstari wa kwanza katika mstari wa pili, au kwa kuendeleza wazo lililosemwa katika mstari uliotangulia katika mstari au mistari inayofuata k.m.:
a. Watu wa Israeli walipotoka Misri
b. Wazawa wa Yakobo walipotoka ugenini (Zab 114:1)
Katika mfano huu wazawa wa Yakobo (b) inawiana na Watu wa Israeli (a) Yakobo na Israeli yakiwa majina ya babu wa Waisraeli au Waebrania; tazama pia walipotoka ugenini (Misri).
a. Mtu mwovu hukopa bila kurudisha
b. Lakini mwadilifu hutoa kwa ukarimu (Zab 37:21)
Hapa pia kuna uhusiano kati ya mstari wa pili (b) na wa kwanza (a) lakini uhusiano huo sio kama tulioelezea hapo kwanza ambapo kulikuwa na uwiano kamili. Hapa mstari wa pili (b) ni kinyume cha mstari wa kwanza (a). Mtindo huu hupatikana mara nyingi katika Zaburi pia lakini ni mtindo unaofaa sana katika misemo ya methali na tenzi za kufunza hekima.
Namna nyingine za kishairi mstari (a) unasema au kutaja kinachofanyika na mstari (b) unatoa sababu au kisa chake. Au (a) ni swali na (b) ni jibu, (a) ni sentensi ya msingi na (b) au na (c) ni marudio yake kwa namna mbalimbali.

Iliyochaguliwa sasa

Zaburi UTANGULIZI: BHN

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia