Ufunuo 17:12-18
Ufunuo 17:12-18 BHN
“Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme ambao bado hawajaanza kutawala. Lakini watapewa mamlaka ya kutawala kwa muda wa saa moja pamoja na yule mnyama. Shabaha ya hawa kumi ni moja, na watampa yule mnyama nguvu na mamlaka yao yote. Watapigana na Mwanakondoo, lakini Mwanakondoo pamoja na wale aliowaita na kuwachagua ambao ni waaminifu, atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme.” Malaika akaniambia pia, “Yale maji uliyoyaona pale alipokaa yule mzinzi: Ni makundi ya watu wa kila taifa, rangi na lugha. Pembe zile kumi ulizoziona na yule mnyama watamchukia huyo mzinzi. Watachukua kila kitu alicho nacho na kumwacha uchi; watakula nyama yake na kumteketeza kwa moto. Maana Mungu ametia mioyoni mwao nia ya kutekeleza shabaha yake, yaani wakubaliane wao kwa wao na kumpa huyo mnyama mamlaka yao ya kutawala, mpaka hapo yale aliyosema Mungu yatakapotimia. “Na yule mwanamke uliyemwona ndio ule mji mkuu ulio na mamlaka juu ya wafalme wa dunia.”