Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 14:1-9

Zekaria 14:1-9 BHN

Tazama, siku ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu inakuja. Siku hiyo, enyi watu wa Yerusalemu, mali yenu itagawanywa mbele ya macho yenu. Mwenyezi-Mungu atayakusanya mataifa yote ili kuushambulia mji wa Yerusalemu. Mji utatekwa, nyumba zenu zitatekwa nyara, na wanawake wenu watanajisiwa. Nusu ya wakazi wa mji watapelekwa uhamishoni, lakini nusu itakayosalia haitachukuliwa nje ya mji. Kisha Mwenyezi-Mungu atatoka na kuyapiga vita mataifa hayo, kama afanyavyo daima siku za vita. Siku hiyo, atasimama kwenye mlima wa mizeituni ulio mashariki ya mji wa Yerusalemu. Mlima huo utagawanywa sehemu mbili na bonde pana sana litatokea toka mashariki hadi magharibi. Nusu moja itaelekea kaskazini na nusu nyingine kusini. Nyinyi mtakimbia kupitia bonde hilo, katikati ya milima miwili ya Mwenyezi-Mungu. Mtakimbia kama wazee wenu walivyokimbia tetemeko la ardhi wakati wa utawala wa mfalme Uzia wa Yuda. Kisha Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, atakuja na watakatifu wote pamoja naye. Wakati huo hakutakuwa baridi wala baridi kali. Mchana utaendelea bila giza kuingia. Wakati huo wajulikana kwa Mwenyezi-Mungu peke yake. Hakutakuwa mchana wala usiku, kwa maana hata saa za jioni mwanga utaendelea kuwapo. Wakati huo, maji ya uhai yatabubujika kutoka mji wa Yerusalemu, na nusu ya maji hayo yatatiririkia kwenye bahari ya mashariki, na nusu nyingine kwenye bahari ya magharibi. Maji hayo yataendelea kububujika wakati wa kiangazi kama yalivyo wakati wa masika. Wakati huo, Mwenyezi-Mungu atakuwa ndiye mfalme pekee wa dunia yote; naye atakuwa ndiye Mwenyezi-Mungu pekee, mmoja tu, na jina lake litakuwa ndilo jina pekee.

Soma Zekaria 14

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Zekaria 14:1-9