Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mambo ya Nyakati 28:1-10

1 Mambo ya Nyakati 28:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Mfalme Daudi akawakusanya huko Yerusalemu wakuu wote wa Israeli: Wa makabila, majemadari na vikosi waliomtumikia mfalme, makamanda wa maelfu, makamanda wa mamia, wasimamizi wa mali zote na ng'ombe wote wa mfalme, na wanawe pamoja na maofisa wa ikulu, mashujaa na askari wote mashuhuri. Ndipo mfalme Daudi akasimama akasemana kusema: “Enyi ndugu zangu na watu wangu, nisikilizeni. Nilikusudia moyoni mwangu kujenga nyumba kwa ajili ya sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, kiti cha kuwekea miguu yake Mungu wetu; na nilifanya maandalizi ya kujenga. Lakini Mungu alinikataza, kwa sababu mimi ni mtu wa vita na nimekwisha mwaga damu nyingi. Lakini Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli alinichagua mimi miongoni mwa jamaa ya baba yangu kuwa mfalme wa Israeli milele. Alilichagua kabila la Yuda liongoze; na kutokana na kabila hilo, aliichagua jamaa ya baba yangu, na miongoni mwa wana wa baba yangu, alipendezwa nami na kuniweka niwe mfalme wa Israeli yote. Mwenyezi-Mungu amenijalia wana wengi, na miongoni mwa hao wote, amemchagua Solomoni mwanangu, aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wake Mwenyezi-Mungu aitawale Israeli. “Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Mwanao Solomoni ndiye atakayenijengea nyumba na nyua zangu, kwa maana nimemchagua yeye awe mwanangu, nami nitakuwa baba yake.’ Nitauimarisha ufalme wake milele ikiwa ataendelea kuzishika kwa dhati amri na sheria zangu kama anavyofanya leo. “Basi sasa, mbele ya kusanyiko hili la Waisraeli wote, jumuiya ya watu wa Mwenyezi-Mungu, na mbele ya Mungu wetu, angalieni mzishike amri zote za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ili mwendelee kuimiliki nchi hii nzuri, na kuwarithisha wazawa wenu baada yenu, hata milele. “Nawe Solomoni mwanangu, umjue Mungu wa baba yako, na umtumikie kwa moyo wako wote na kwa nia thabiti; yeye Mwenyezi-Mungu huchunguza mioyo na anafahamu mipango na fikira za binadamu. Ukimtafuta yeye, utamwona; lakini ukimwacha, atakutupilia mbali milele. Basi, ujihadhari na kukumbuka ya kwamba, Mwenyezi-Mungu amekuchagua wewe umjengee nyumba ya ibada. Uwe hodari ukatende hivyo.”

1 Mambo ya Nyakati 28:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Kisha Daudi akawakusanya huko Yerusalemu wakuu wote wa Israeli, wakuu wa kabila, na makamanda wa vikosi wenye kumtumikia mfalme kwa zamu, na makamanda wa maelfu, na makamanda wa mamia, na wenye kutawala juu ya mali na milki za mfalme, na za wanawe, pamoja na matowashi, na mashujaa, naam, wanaume mashujaa wote. Ndipo Daudi mfalme akasimama kwa miguu yake, akasema, Nisikilizeni, ndugu zangu, na watu wangu; Mimi nilikuwa na nia ya kuijenga nyumba ya kuliweka sanduku la Agano la BWANA, na kiti cha kuwekea miguu cha Mungu wetu; hata nilikuwa nimejitayarisha kujenga. Lakini Mungu akaniambia, Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umekuwa mtu wa vita, nawe umemwaga damu. Walakini BWANA, Mungu wa Israeli, alinichagua katika nyumba yote ya babangu kuwa mfalme juu ya Israeli milele, kwa kuwa amemchagua Yuda awe mkuu; na katika nyumba ya Yuda, alichagua nyumba ya babangu, na miongoni mwa wana wa babangu, aliniridhia mimi ili kunitawaza niwe mfalme juu ya Israeli wote; tena katika wana wangu wote (kwani BWANA amenipa wana wengi), amemchagua Sulemani mwanangu ili aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wa BWANA, juu ya Israeli. Akaniambia, Sulemani, mwanao, ndiye atakayeijenga nyumba yangu na nyua zangu; kwa kuwa nimemchagua awe mwanangu, nami nitakuwa babaye. Na ufalme wake nitauimarisha milele, akiendelea kuzitenda amri zangu na hukumu zangu kwa dhati, kama hivi leo. Basi sasa, machoni pa Israeli wote, hilo kusanyiko la BWANA, na masikioni pa Mungu wetu, shikeni na kuzifuata amri zote za BWANA, Mungu wenu, ili mpate kuimiliki nchi hii njema, na kuwarithisha wana wenu baada yenu hata milele. Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa BWANA huchunguza mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, atakuwa nawe; ukimwacha, atakutupa milele. Jihadhari basi; kwani BWANA amekuchagua wewe ili ujenge nyumba itakayokuwa mahali patakatifu; uwe hodari ukatende hivyo.

1 Mambo ya Nyakati 28:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Kisha Daudi akawakusanya huko Yerusalemu wakuu wote wa Israeli, wakuu wa kabila, na maakida wa vikosi wenye kumtumikia mfalme kwa zamu, na maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, na wenye kutawala juu ya mali na milki za mfalme, na za wanawe, pamoja na matowashi, na mashujaa, naam, waume mashujaa wote. Ndipo Daudi mfalme akasimama kwa miguu yake, akasema, Nisikilizeni, ndugu zangu, na watu wangu; Mimi nalikuwa na nia ya kuijenga nyumba ya kustarehe kwa ajili ya sanduku la agano la BWANA, na kiti cha kuwekea miguu yake cha Mungu wetu; hata nalikuwa nimeweka tayari kwa kujenga. Lakini Mungu akaniambia, Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umekuwa mtu wa vita, nawe umemwaga damu. Walakini BWANA, Mungu wa Israeli, alinichagua katika nyumba yote ya babangu kuwa mfalme juu ya Israeli milele, kwa kuwa amemchagua Yuda awe mkuu; na katika nyumba ya Yuda, alichagua nyumba ya babangu, na miongoni mwa wana wa babangu, aliniridhia mimi ili kunitawaza niwe mfalme juu ya Israeli wote; tena katika wana wangu wote (kwani BWANA amenipa wana wengi), amemchagua Sulemani mwanangu ili aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wa BWANA, juu ya Israeli. Akaniambia, Sulemani, mwanao, ndiye atakayeijenga nyumba yangu na nyua zangu; kwa kuwa nimemchagua awe mwanangu, nami nitakuwa babaye. Na ufalme wake nitauweka imara milele, akijitia kwa bidii kuzitenda amri zangu na hukumu zangu, kama hivi leo. Basi sasa, machoni pa Israeli wote, hilo kusanyiko la BWANA, na masikioni pa Mungu wetu, angalieni na kuzitafuta amri zote za BWANA, Mungu wenu, ili mpate kuimiliki nchi hii njema, na kuwarithisha wana wenu baada yenu hata milele. Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa BWANA hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele. Jihadhari basi; kwani BWANA amekuchagua wewe ili ujenge nyumba itakayokuwa mahali patakatifu; uwe hodari ukatende hivyo.

1 Mambo ya Nyakati 28:1-10 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)

Daudi akawaita maafisa wote wa Israeli wakusanyike huko Yerusalemu: yaani maafisa walio juu ya makabila, majemadari wa vikosi katika utumishi wa mfalme, majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia, maafisa wanaosimamia mali yote na mifugo ya mfalme na wanawe, wakiwemo maafisa wa jumba la kifalme, mashujaa na wapiganaji hodari wote. Mfalme Daudi akainuka na kusema: “Nisikilizeni ndugu zangu, nanyi watu wangu. Nilikuwa na nia ya kujenga nyumba ili iwe mahali pa kukaa Sanduku la Agano la BWANA, kwa ajili ya kuwa mahali pa kuwekea miguu ya Mungu wetu, nami nikafanya maandalizi ya kuijenga. Lakini Mungu akaniambia, ‘Wewe hutajenga nyumba kwa Jina langu, kwa sababu wewe umekuwa mtu wa vita na umemwaga damu.’ “Hata hivyo, BWANA, Mungu wa Israeli, alinichagua mimi kutoka jamaa zangu wote niwe mfalme juu ya Israeli milele. Alimchagua Yuda kuwa kiongozi, na kutoka nyumba ya Yuda akaichagua jamaa yangu, na kutoka wana wa baba yangu ikampendeza kunifanya niwe mfalme juu ya Israeli yote. Miongoni mwa wanangu wote, naye BWANA amenipa wengi, amemchagua Sulemani mwanangu ili kukikalia kiti cha utawala cha ufalme wa BWANA juu ya Israeli. Aliniambia, ‘Sulemani mwanao ndiye atakayejenga nyumba yangu na nyua zangu, kwa maana nimemchagua yeye kuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake. Nitauimarisha ufalme wake milele kama akiendelea kuzishika amri zangu na sheria zangu, kama afanyavyo hivi leo.’ “Hivyo basi ninawaagiza mbele za Israeli yote na kusanyiko hili la BWANA, naye Mungu wetu akiwa anasikia: Kuweni na bidii kuzifuata amri za BWANA Mungu wenu, ili mpate kumiliki nchi hii nzuri, na kuwaachia wana wenu kuwa urithi milele. “Nawe Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa kujitoa kwa moyo wote na kwa nia ya kumkubali, kwa maana BWANA huuchunguza kila moyo na kujua kila kusudi la kila fikira. Ukimtafuta, ataonekana kwako; bali ukimwacha, yeye atakukataa milele. Angalia basi, kwa maana BWANA amekuchagua wewe ili ujenge Hekalu kuwa mahali patakatifu. Uwe hodari ukafanye kazi hiyo.”