1 Mambo ya Nyakati 29:20-30
1 Mambo ya Nyakati 29:20-30 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha, mfalme Daudi aliwaambia wote waliokusanyika, “Msifuni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.” Na wote waliokusanyika wakamtukuza Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao, wakamsujudia na kumwabudu Mwenyezi-Mungu na kumtolea mfalme Daudi heshima. Wakamtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Siku ya pili yake wakamtolea sadaka za kuteketezwa: Mafahali 1,000, wanakondoo 1,000, pamoja na sadaka zao za vinywaji na tambiko nyingi kwa ajili ya Waisraeli wote. Basi siku hiyo walikula na kunywa kwa furaha kuu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Wakamtawaza Solomoni mwana wa Daudi, mara ya pili. Wakampaka mafuta awe mtawala kwa jina la Mwenyezi-Mungu, na Sadoki awe kuhani. Ndipo Solomoni akaketi katika kiti cha enzi cha Mwenyezi-Mungu, badala ya Daudi baba yake. Naye akafanikiwa, na taifa lote la Israeli likamtii. Viongozi wote, mashujaa na wana wote wa Daudi wakajiweka chini ya mfalme Solomoni. Mwenyezi-Mungu akampa Solomoni sifa nzuri machoni pa Waisraeli wote, akampa fahari ya kifalme ipitayo fahari ya mfalme awaye yote aliyeitawala Israeli kabla yake. Basi Daudi, mwana wa Yese, akawa mfalme juu ya Israeli yote. Na muda aliotawala juu ya Israeli ulikuwa miaka arubaini; miaka saba alitawala huko Hebroni na miaka thelathini na mitatu alitawala huko Yerusalemu. Alikufa akiwa mzee mwenye miaka mingi, ameshiba siku, akiwa na mali na heshima. Solomoni mwanawe, akawa mfalme badala yake. Habari za mfalme Daudi toka mwanzo hadi mwisho, zimeandikwa katika kumbukumbu za Samueli mwonaji, katika kumbukumbu za nabii Nathani na katika kumbukumbu za Gadi mwonaji. Hizo zasema pamoja na mambo ya utawala wake, uwezo wake, na mambo yaliyompata yeye, Waisraeli, na falme zote nchini.
1 Mambo ya Nyakati 29:20-30 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini BWANA, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao, wakainamisha vichwa vyao, wakamsujudia BWANA, na mfalme naye. Siku ya pili yake, wakamtolea BWANA dhabihu, wakamchinjia BWANA sadaka ya kuteketezwa, yaani, ng'ombe elfu moja, na kondoo dume elfu moja, na wana-kondoo elfu moja, pamoja na sadaka zao za vinywaji, na dhabihu nyingi kwa ajili ya Israeli wote; wakala na kunywa mbele za BWANA siku ile, kwa furaha kuu. Wakamtawaza Sulemani, mwana wa Daudi, mara ya pili, wakamtia mafuta mbele za BWANA, awe mkuu, na Sadoki awe kuhani. Ndipo Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha BWANA, awe mfalme badala ya Daudi babaye, akafanikiwa; nao Israeli wote wakamtii. Nao wakuu wote, na mashujaa, na wana wote wa mfalme Daudi nao, wakaahidi kuwa watiifu kwa mfalme Sulemani. Naye BWANA akamtukuza Sulemani mno machoni pa Israeli wote, akampa fahari ya kifalme ya kumpita mfalme awaye yote aliyekuwa kabla yake katika Israeli. Basi Daudi, mwana wa Yese, akawa mfalme juu ya Israeli wote. Na wakati aliotawala juu ya Israeli, ulikuwa miaka arubaini; miaka saba alitawala Hebroni, na miaka thelathini na mitatu akatawala Yerusalemu. Akafa akiwa mzee sana, mwenye maisha marefu, mali na heshima; naye Sulemani mwanawe akatawala badala yake. Basi habari za mfalme Daudi, mwanzo hadi mwisho, angalia, zimeandikwa katika kumbukumbu za Samweli, mwonaji, na katika kumbukumbu za Nathani, nabii, na katika kumbukumbu za Gadi, mwonaji; zikisimulia kuhusu kutawala kwake kote na nguvu zake, na mambo yote yaliyompata yeye, na Israeli, na falme zote za nchi.
1 Mambo ya Nyakati 29:20-30 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini BWANA, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao, wakainama vichwa vyao, wakamsujudia BWANA, na mfalme naye. Wakamtolea BWANA dhabihu, wakamchinjia BWANA sadaka za kuteketezwa, siku ya pili yake, yaani, ng’ombe elfu, na kondoo waume elfu, na wana-kondoo elfu, pamoja na sadaka zao za vinywaji, na dhabihu nyingi kwa ajili ya Israeli wote; wakala na kunywa mbele za BWANA siku ile, kwa furaha kuu. Wakamtawaza Sulemani, mwana wa Daudi, mara ya pili, wakamtia mafuta mbele za BWANA, awe mkuu, na Sadoki awe kuhani. Ndipo Sulemani akaketi katika kiti cha enzi cha BWANA, awe mfalme badala ya Daudi babaye, akafanikiwa; nao Israeli wote wakamtii. Nao wakuu wote, na mashujaa, na wana wote wa mfalme Daudi nao, wakajitia chini ya mfalme Sulemani. Naye BWANA akamtukuza Sulemani mno machoni pa Israeli wote, akampa fahari ya kifalme ya kumpita mfalme awaye yote aliyekuwa kabla yake katika Israeli. Basi Daudi, mwana wa Yese, akawa mfalme juu ya Israeli wote. Na wakati aliotawala juu ya Israeli, ulikuwa miaka arobaini; miaka saba alitawala Hebroni, na miaka thelathini na mitatu akatawala Yerusalemu. Akafa mwenye umri mwema, ameshiba siku, na mali, na heshima; naye Sulemani mwanawe akamiliki badala yake. Basi habari za mfalme Daudi, mwanzo na mwisho, angalia, zimeandikwa katika tarehe ya Samweli, mwonaji, na katika tarehe ya Nathani, nabii, na katika tarehe ya Gadi, mwonaji; pamoja na kutawala kwake kote na nguvu zake, nazo zamani zilizompata yeye, na Israeli, na falme zote za nchi.
1 Mambo ya Nyakati 29:20-30 Neno: Bibilia Takatifu 2025 (NENO)
Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, “Mhimidini BWANA Mungu wenu.” Hivyo wote wakamhimidi BWANA, Mungu wa baba zao. Wakasujudu, na nyuso zao zikagusa chini mbele za BWANA na mfalme. Siku ya pili yake, wakamtolea BWANA dhabihu na sadaka za kuteketezwa: mafahali elfu moja, kondoo dume elfu moja, na wana-kondoo dume elfu moja, pamoja na sadaka za vinywaji, na sadaka nyingine nyingi sana kwa ajili ya Israeli yote. Wakala na kunywa kwa furaha kubwa mbele za BWANA siku ile. Wakamtawaza Sulemani mwana wa Daudi mara ya pili kuwa mfalme, wakampaka mafuta mbele za BWANA ili awe mfalme na Sadoki kuwa kuhani. Sulemani akaketi kwenye kiti cha enzi cha BWANA kuwa mfalme mahali pa Daudi baba yake. Akafanikiwa sana, na Waisraeli wote wakamtii. Maafisa wote na mashujaa, pamoja na wana wote wa Daudi, wakaahidi kumtii Mfalme Sulemani. BWANA akamtukuza sana Sulemani mbele ya Waisraeli wote na kumvika fahari ya kifalme ambayo hakuna mfalme yeyote wa Israeli kabla yake aliwahi kuwa nayo. Daudi mwana wa Yese alikuwa mfalme wa Israeli yote. Alitawala Israeli kwa miaka arobaini: huko Hebroni alitawala miaka saba, na katika Yerusalemu akatawala miaka thelathini na tatu. Daudi akafa akiwa mzee mwenye umri mwema, akiwa ameshiba siku, utajiri na heshima. Naye Sulemani mwanawe akawa mfalme baada yake. Kuhusu matukio ya utawala wa Mfalme Daudi, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa katika kumbukumbu za mwonaji Samweli, na kumbukumbu za nabii Nathani na kumbukumbu za mwonaji Gadi, pamoja na habari zote za utawala wake, nguvu zake na matukio yaliyompata yeye, na Israeli, na falme za nchi nyingine zote.