1 Wakorintho 6:12-20
1 Wakorintho 6:12-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Mtu anaweza kusema: “Kwangu mimi kila kitu ni halali.” Sawa; lakini si kila kitu kinafaa. Nakubali kwamba kila kitu ni halali kwangu lakini sitaki kutawaliwa na kitu chochote. Unaweza kusema: “Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula.” Sawa; lakini Mungu ataviharibu vyote viwili. Mwili wa mtu si kwa ajili ya uzinzi bali ni kwa ajili ya kumtumikia Bwana, naye Bwana ni kwa ajili ya mwili. Basi, Mungu aliyemfufua Bwana kutoka wafu atatufufua nasi pia kwa nguvu yake. Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya mwili wa Kristo? Je, mnadhani naweza kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuifanya kuwa sehemu ya mwili wa kahaba? Hata kidogo! Maana, kama mjuavyo, anayeungana na kahaba huwa mwili mmoja naye – kama ilivyoandikwa: “Nao wawili watakuwa mwili mmoja.” Lakini aliyejiunga na Bwana huwa roho moja naye. Jiepusheni kabisa na uzinzi. Dhambi nyingine zote hutendwa nje ya mwili lakini mzinzi hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe. Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, ambaye mlimpokea kutoka kwa Mungu? Nyinyi basi, si mali yenu wenyewe. Mlinunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo, itumieni miili yenu kwa ajili ya kumtukuza Mungu.
1 Wakorintho 6:12-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu chochote. Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula. Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili. Naye Mungu alimfufua Bwana, na tena atatufufua sisi kwa uweza wake. Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? La hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye. Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.
1 Wakorintho 6:12-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote. Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula. Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili. Naye Mungu alimfufua Bwana, na tena atatufufua sisi kwa uweza wake. Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye. Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yen
1 Wakorintho 6:12-20 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
“Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini si vitu vyote vyenye faida. “Vitu vyote ni halali kwangu”: lakini sitatawaliwa na kitu chochote. “Chakula ni cha tumbo, na tumbo ni la chakula”: lakini Mungu ataviangamiza vyote viwili. Mwili sio kwa ajili ya zinaa, bali kwa ajili ya Bwana Isa, na Bwana Isa kwa ajili ya mwili. Naye Mungu aliyemfufua Bwana Isa kutoka kwa wafu atatufufua sisi pia kwa uweza wake. Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya Al-Masihi mwenyewe? Je, nichukue viungo vya mwili wa Al-Masihi na kuviunganisha na mwili wa kahaba? La hasha! Hamjui kwamba aliyeungwa na kahaba anakuwa mwili mmoja naye? Kwa kuwa imenenwa, “Hao wawili watakuwa mwili mmoja.” Lakini mtu aliyeungwa na Bwana Isa anakuwa roho moja naye. Ikimbieni zinaa. Dhambi zingine zote atendazo mtu ziko nje ya mwili wake, lakini yeye aziniye hutenda dhambi ndani ya mwili wake mwenyewe. Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu wa Mungu akaaye ndani yenu, ambaye mmepewa na Mungu? Ninyi si mali yenu wenyewe, kwa maana mmenunuliwa kwa gharama. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu katika miili yenu.