1 Wafalme 11:1-8
1 Wafalme 11:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, na wa mataifa BWANA aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda. Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wakeze wakamgeuza moyo. Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni. Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, wala hakumfuata BWANA kwa utimilifu, kama Daudi baba yake. Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu.
1 Wafalme 11:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Solomoni alipenda sana wanawake wa kigeni: Binti Farao, wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni, na Wahiti; wanawake wa mataifa ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amewakataza Waisraeli akisema, “Msioe kwao wala wao wasioe kwenu kwa sababu wanawake hao watapotosha mioyo yenu ili muitumikie miungu yao.” Solomoni aliwapenda sana wanawake hao. Solomoni akawa na wanawake 700, wote mabinti wa kifalme; na masuria 300. Hao wanawake wakampotosha. Maana, alipokuwa mzee, wake zake walimpotosha hata akaitumikia miungu mingine, wala hakuwa mwaminifu kabisa kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, kama baba yake Daudi alivyokuwa mwaminifu. Solomoni alimtumikia Ashtarothi aliyekuwa mungu wa kike wa Wasidoni, na alimfuata Milkomu chukizo la Waamoni. Hivyo, Solomoni alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, wala hakufuata kwa ukamilifu matakwa ya Mwenyezi-Mungu kama baba yake Daudi alivyokuwa amefanya. Juu ya mlima ulio mashariki ya Yerusalemu, Solomoni alijenga mahali pa kumtambikia Kemoshi, chukizo la Wamoabu, na mahali pa kumtambikia Moleki, chukizo la Waamoni. Kadhalika, aliwajengea wake zake wote wa kigeni mahali pa kufukizia ubani na kuitambikia miungu yao.
1 Wafalme 11:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mfalme Sulemani akawapenda wanawake wengi wageni, pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi, na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni, na wa Wahiti, na wa mataifa BWANA aliyowaambia wana wa Israeli, Msiingie kwao, wala wasiingie kwenu; kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao. Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda. Akawa na wake mia saba binti za kifalme, na masuria mia tatu; nao wake zake wakamgeuza moyo. Maana ikawa, Sulemani alipokuwa mzee, wake zake wakamgeuza moyo wake, afuate miungu mingine, wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. Kwa kuwa Sulemani akamfuata Ashtorethi, mungu wa kike wa Wasidoni na Milkomu, chukizo la Waamoni. Sulemani akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, wala hakumfuata BWANA kwa utimilifu, kama Daudi baba yake. Sulemani akamjengea Kemoshi, chukizo la Wamoabi, mahali pa juu, katika mlima uliokabili Yerusalemu, na Moleki, chukizo la wana wa Amoni. Na kadhalika ndivyo alivyowafanyia wake zake wa nchi za kigeni, waliofukiza uvumba, wakawatolea miungu yao dhabihu.
1 Wafalme 11:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hata hivyo, Mfalme Solomoni akawapenda wanawake wengi wa kigeni zaidi, mbali na binti Farao: wanawake wa Wamoabu, Waamoni, Waedomu, Wasidoni na Wahiti. Walitoka katika mataifa ambayo BWANA aliwaambia Waisraeli, “Msije mkaoana nao, kwa kuwa hakika wataigeuza mioyo yenu mgeukie miungu yao.” Hata hivyo, Solomoni akakaza kuwapenda. Alikuwa na wake 700 mabinti wa uzao wa kifalme, na masuria 300, nao wake zake wakampotosha. Kadiri Solomoni alivyozidi kuzeeka, wake zake wakaugeuza moyo wake kuelekea miungu mingine, na moyo wake haukujitolea kikamilifu kwa BWANA Mungu wake, kama ulivyokuwa moyo wa Daudi baba yake. Solomoni akafuata Ashtorethi mungu mke wa Wasidoni, na Moleki mungu aliyekuwa chukizo la Waamoni. Kwa hiyo Solomoni akafanya uovu machoni pa BWANA; hakumfuata BWANA kikamilifu kama alivyofanya Daudi baba yake. Kwenye kilima mashariki mwa Yerusalemu, Solomoni akajenga mahali pa juu kwa ajili ya Kemoshi chukizo la Wamoabu, na kwa Moleki mungu chukizo la Waamoni. Akafanya hivyo kwa wake zake wote wa kigeni, ambao walifukiza uvumba na kutoa dhabihu kwa miungu yao.