Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 11:26-43

1 Wafalme 11:26-43 Biblia Habari Njema (BHN)

Yeroboamu mwana wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumishi wa Solomoni, ambaye mama yake mjane, aliitwa Zerua, pia alimwasi mfalme. Kisa cha uasi huo ni hiki: Solomoni alipokuwa akishughulika na kusawazisha sehemu ya Milo, na kuimarisha kuta za mji wa baba yake Daudi, Yeroboamu alionekana kuwa kijana hodari na shujaa. Ndipo Solomoni alipoona kwamba huyo kijana alikuwa mwenye bidii, akamweka awe msimamizi wa kazi za kulazimishwa zilizofanywa na watu wa ukoo wa Yosefu. Siku moja, Yeroboamu alipokuwa akisafiri kutoka Yerusalemu, nabii Ahiya wa Shilo alikutana naye njiani. Ahiya alikuwa amevaa vazi jipya. Wote wawili walikuwa peke yao mashambani. Mara, Ahiya akalivua vazi lake jipya, akalirarua vipande kumi na viwili, halafu akamwambia Yeroboamu, “Jitwalie vipande kumi maana Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Tazama, karibu nitaurarua ufalme na kuuondoa mikononi mwa Solomoni, nami nitakupa wewe makabila kumi.’ Lakini yeye nitamwachia kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya mji wa Yerusalemu ambao nimeuchagua kuwa wangu katika makabila yote ya Israeli. Nitafanya hivyo kwa sababu Solomoni ameniacha, akaabudu miungu ya kigeni: Ashtarothi mungu wa kike wa Wasidoni, Kemoshi, mungu wa Wamoabu na Milkomu mungu wa Waamoni. Solomoni ameniasi, ametenda maovu mbele yangu, na wala hakutii sheria zangu na maagizo yangu kama Daudi baba yake alivyofanya. Hata hivyo, sitamnyanganya milki yote, wala sitamwondolea mamlaka maishani mwake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi ambaye nilimchagua, na ambaye alifuata amri zangu na maongozi yangu. Lakini, nitamnyanganya mwanawe ufalme huo, nami nitakupatia wewe Yeroboamu makabila kumi. Huyo mwanawe Solomoni nitamwachia kabila moja, ili wakati wote mzawa wa mtumishi wangu Daudi awe anatawala Yerusalemu, awe taa inayoangaza daima mbele yangu katika mji ambao nimeuchagua uwe mahali pa kuniabudia. Basi, wewe Yeroboamu, nitakufanya kuwa mfalme wa Israeli, nawe utatawala kama upendavyo. Na kama utazingatia yote nitakayokuamuru, kama utaishi kulingana na matakwa yangu, kama utatenda mema mbele zangu kwa kushika maongozi yangu na amri zangu, kama mtumishi wangu Daudi alivyofanya, mimi nitakuwa pamoja nawe daima. Na nitakupatia nchi ya Israeli na kuufanya utawala wako uwe thabiti kama nilivyomfanyia Daudi. Kutokana na hayo, nitawaadhibu wazawa wa Daudi, lakini si daima.” Kwa sababu hiyo, Solomoni alijaribu kumuua Yeroboamu; lakini Yeroboamu akakimbilia Misri kwa Shishaki mfalme wa Misri, akakaa huko mpaka Solomoni alipofariki. Mambo mengine ya Solomoni, yote aliyotenda na hekima yake, yameandikwa katika Kitabu cha Matendo ya Solomoni. Kwa muda wa miaka arubaini, Solomoni aliitawala nchi yote ya Israeli; makao yake yakiwa Yerusalemu. Hatimaye, Solomoni alifariki, akazikwa katika mji wa baba yake Daudi. Rehoboamu, mwanawe Solomoni, akatawala mahali pake.

1 Wafalme 11:26-43 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Na Yeroboamu wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumwa wake Sulemani; ambaye jina lake mamaye aliitwa Serua, mwanamke aliyefiwa na mumewe; yeye naye akamwasi mfalme. Na hii ndiyo sababu ya yeye kumwasi mfalme. Sulemani aliijenga Milo, akapafunga palipobomoka pa mji wa baba yake Daudi. Na huyo Yeroboamu alikuwa mtu hodari, shujaa; Sulemani akaona ya kuwa kijana huyo ni mtu mwenye bidii, akamweka juu ya kazi yote ya nyumba ya Yusufu. Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili. Akamwambia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe makabila kumi, (lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu mji ule niliouchagua katika miji yote ya makabila ya Israeli); kwa sababu wameniacha mimi wakaabudu Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Kemoshi, mungu wa Wamoabi, na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni wala hawakuenda katika njia zangu, kutenda mema machoni pangu, kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, kama Daudi baba yake. Lakini sitauondoa ufalme wote katika mkono wake; bali nitamfanya awe mkuu siku zote za maisha yake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi niliyemchagua kwa maana alizishika amri zangu na sheria zangu, ila nitauondoa ufalme katika mkono wa mwanawe, nami nitakupa wewe makabila kumi. Nami nitampa mwana wake kabila moja, ili Daudi, mtumishi wangu, apate kuwa na taa siku zote mbele zangu katika Yerusalemu, mji ule niliouchagua niweke jina langu huko. Nami nitakutwaa wewe, nawe utatawala kama roho yako inavyotamani, nawe utakuwa mfalme juu ya Israeli. Tena itakuwa, ukiyasikia yote nitakayokuamuru, na kuenda katika njia zangu, na kutenda yaliyo mema machoni pangu, ili kuzishika amri zangu na hukumu zangu kama Daudi mtumishi wangu alivyotenda, basi, nitakuwa pamoja nawe, nitakujengea nyumba iliyo imara, kama nilivyomjengea Daudi, nami nitakupa wewe Israeli. Tena nitawatesa wazao wa Daudi kwa sababu hii, lakini si daima. Basi Sulemani akataka kumwua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akaondoka, akakimbilia Misri, kwa Shishaki, mfalme wa Misri, akakaa katika Misri hata wakati wa kufa kwake Sulemani. Nayo yaliyosalia ya Sulemani, mambo yake na yote aliyoyafanya, na hekima yake, je! Hayo siyo yaliyoandikwa kitabuni mwa mambo yake Sulemani? Na siku alizotawala Sulemani katika Yerusalemu juu ya Israeli wote zilikuwa miaka arubaini. Naye Sulemani akalala na baba zake, akazikwa katika mji wa Daudi baba yake; na Rehoboamu mwanawe akatawala mahali pake.

1 Wafalme 11:26-43 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Na Yeroboamu wa Nebati, Mwefraimu wa Sereda, mtumwa wake Sulemani; ambaye jina lake mamaye aliitwa Serua, mwanamke aliyefiwa na mumewe; yeye naye akainua mkono wake juu ya mfalme. Na hii ndiyo sababu ya yeye kumwinulia mfalme mkono. Sulemani aliijenga Milo, akapafunga palipobomoka pa mji wa baba yake Daudi. Na huyo Yeroboamu alikuwa mtu hodari, shujaa; Sulemani akaona ya kuwa kijana huyo ni mtu mwenye bidii, akamweka juu ya kazi yote ya nyumba ya Yusufu. Ikawa zamani zile Yeroboamu alipokuwa akitoka katika Yerusalemu, nabii Ahiya, Mshiloni, alikutana naye njiani; naye Ahiya amevaa vazi jipya, na hao wawili walikuwa peke yao mashambani. Ahiya akalishika lile vazi jipya alilokuwa amelivaa, akalirarua vipande kumi na viwili. Akamwambia Yeroboamu, Twaa wewe vipande kumi, maana BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nitaurarua ufalme, na kuuondoa katika mkono wa Sulemani, nami nitakupa wewe kabila kumi, (lakini yeye atakuwa na kabila moja kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi, na kwa ajili ya Yerusalemu mji ule niliouchagua katika miji yote ya kabila za Israeli); kwa sababu wameniacha mimi wakaabudu Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Kemoshi, mungu wa Wamoabi, na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni wala hawakuenda katika njia zangu, kutenda mema machoni pangu, kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, kama Daudi baba yake. Walakini sitauondoa ufalme wote katika mkono wake; lakini nitamfanya awe mkuu siku zote za maisha yake, kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi niliyemchagua kwa maana alizishika amri zangu na sheria zangu, lakini nitauondoa ufalme katika mkono wa mwanawe, nami nitakupa wewe kabila kumi. Nami nitampa mwana wake kabila moja, ili Daudi, mtumishi wangu, apate kuwa na taa siku zote mbele zangu katika Yerusalemu, mji ule niliouchagua niweke jina langu huko. Nami nitakutwaa wewe, nawe utatawala kama roho yako inavyotamani, nawe utakuwa mfalme juu ya Israeli. Tena itakuwa, ukiyasikia yote nitakayokuamuru, na kuenda katika njia zangu, na kutenda yaliyo mema machoni pangu, ili kuzishika amri zangu na hukumu zangu kama Daudi mtumishi wangu alivyotenda, basi, nitakuwa pamoja nawe, nitakujengea nyumba iliyo imara, kama nilivyomjengea Daudi, nami nitakupa wewe Israeli. Tena nitawatesa wazao wa Daudi kwa sababu hii, lakini si daima. Basi Sulemani akataka kumwua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akaondoka, akakimbilia Misri, kwa Shishaki, mfalme wa Misri, akakaa katika Misri hata wakati wa kufa kwake Sulemani. Nayo yaliyosalia ya Sulemani, mambo yake na yote aliyoyafanya, na hekima yake, je! Hayo siyo yaliyoandikwa kitabuni mwa mambo yake Sulemani? Na siku alizotawala Sulemani katika Yerusalemu juu ya Israeli wote zilikuwa miaka arobaini. Naye Sulemani akalala na baba zake, akazikwa katika mji wa Daudi baba yake; na Rehoboamu mwanawe akatawala mahali pake.

1 Wafalme 11:26-43 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Pia, Yeroboamu mwana wa Nebati aliasi dhidi ya mfalme. Alikuwa mmoja wa maafisa wa Solomoni, Mwefraimu kutoka Sereda, ambaye mama yake alikuwa mjane aliyeitwa Serua. Haya ndiyo maelezo ya jinsi alivyomwasi mfalme: Solomoni alikuwa amejenga Milo naye akawa ameziba mwanya katika ukuta wa mji wa Daudi baba yake. Basi Yeroboamu alikuwa mtu shujaa na hodari, naye Solomoni alipoona jinsi kijana alivyofanya kazi yake, akamweka kuwa kiongozi wa kazi yote ya mikono ya nyumba ya Yosefu. Karibu na wakati ule Yeroboamu alikuwa anatoka nje ya Yerusalemu, Ahiya nabii Mshiloni akakutana naye njiani, akiwa amevaa joho jipya. Hawa wawili walikuwa peke yao mashambani, naye Ahiya akachukua joho jipya alilokuwa amevaa akalirarua vipande kumi na viwili. Kisha akamwambia Yeroboamu, “Chukua vipande kumi kwa ajili yako, kwa kuwa hivi ndivyo BWANA, Mungu wa Israeli asemavyo: ‘Tazama, ninakwenda kuuchana ufalme kutoka mikononi mwa Solomoni na kukupa wewe makabila kumi. Lakini kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi na mji wa Yerusalemu, ambao nimeuchagua miongoni mwa makabila yote ya Israeli, atakuwa na kabila moja. Nitafanya hivi kwa sababu wameniacha mimi na kuabudu Ashtorethi mungu mke wa Wasidoni, Kemoshi mungu wa Wamoabu, na Moleki mungu wa Waamoni, nao hawakwenda katika njia zangu ili kufanya yaliyo sawa machoni pangu, wala kushika amri na sheria zangu kama Daudi, babaye Solomoni, alivyofanya. “ ‘Lakini sitauondoa ufalme wote kutoka mikononi mwa Solomoni, nimemfanya mtawala siku zote za maisha yake kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, niliyemchagua na ambaye aliyatunza maagizo na amri zangu. Nitauondoa ufalme kutoka mikononi mwa mwanawe na kukupa wewe makabila kumi. Nitampa mwanawe kabila moja ili kwamba Daudi mtumishi wangu awe na taa mbele zangu daima katika Yerusalemu, mji ambao nimeuchagua kuweka Jina langu. Hata hivyo, kukuhusu wewe Yeroboamu, nitakutwaa, nawe utatawala juu ya yote yale moyo wako unayotamani, utakuwa mfalme juu ya Israeli. Ikiwa utafanya kila nitakalokuamuru, kuenenda katika njia zangu na kufanya yaliyo sawa mbele za macho yangu kwa kuzishika amri zangu na maagizo yangu kama alivyofanya Daudi mtumishi wangu, nitakuwa pamoja nawe. Nitakujengea ufalme utakaodumu kama ule niliomjengea Daudi, nami nitakupa Israeli. Nitawatesa wazao wa Daudi kwa ajili ya hili, lakini siyo milele.’ ” Solomoni akajaribu kumuua Yeroboamu, lakini Yeroboamu akakimbilia Misri, kwa Mfalme Shishaki, naye akakaa huko mpaka Solomoni alipofariki. Kwa habari za matukio mengine ya utawala wa Solomoni, yote aliyoyafanya na hekima aliyoionyesha, je hayakuandikwa yote katika kitabu cha matendo cha Solomoni? Solomoni alitawala Israeli yote miaka arobaini, akiwa Yerusalemu. Kisha Solomoni akalala pamoja na baba zake, naye akazikwa katika mji wa Daudi baba yake. Naye Rehoboamu mwanawe akawa mfalme baada yake.