1 Wafalme 14:1-11
1 Wafalme 14:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)
Wakati huo, Abiya mwana wa mfalme Yeroboamu, akawa mgonjwa. Yeroboamu akamwambia mkewe, “Jisingizie kuwa mwingine, uende mjini Shilo anakokaa nabii Ahiya aliyesema kwamba mimi nitakuwa mfalme wa Israeli. Mpelekee mikate kumi, maandazi kadha, na asali chupa moja. Yeye atakuambia yatakayompata mtoto wetu.” Basi, mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda Shilo nyumbani kwa Ahiya. Wakati huo, Ahiya alikuwa hawezi tena kuona sawasawa kwa sababu ya uzee. Mwenyezi-Mungu alikuwa amekwisha mwambia Ahiya kwamba mke wa Yeroboamu alikuwa njiani, anakuja kumwuliza yatakayompata mwanawe mgonjwa, na jinsi atakavyomjibu. Mkewe Yeroboamu alipofika, alijisingizia kuwa mtu mwingine. Lakini Ahiya alipomsikia anaingia mlangoni, alisema, “Karibu ndani mke wa Yeroboamu. Lakini mbona unajisingizia kuwa mtu mwingine? Ninao ujumbe usio mzuri kwako! Nenda ukamwambie Yeroboamu kwamba Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: ‘Nilikuteua miongoni mwa watu, nikakufanya kuwa kiongozi wa watu wangu, Israeli; nikaurarua ufalme utoke kwa wazawa wa Daudi, nikakupa wewe. Lakini wewe ni kinyume kabisa cha mtumishi wangu Daudi ambaye alizishika amri zangu, akafuata matakwa yangu kwa moyo wake wote na kutenda tu yaliyo sawa mbele ya macho yangu. Wewe umetenda uovu mbaya zaidi kuliko waliotenda wale waliokutangulia; wewe umenikasirisha kwa kujitengenezea miungu mingine na sanamu za kufua, kisha umeniacha. Haya basi, sasa nitailetea balaa jamaa hii yake, Yeroboamu, nitawaua wanaume wote wa jamaa zake katika Israeli, awe mtumwa au huru. Jamaa wake wote nitawateketeza kama mtu ateketezavyo mavi, mpaka yatoweke. Yeyote aliye wa jamaa ya Yeroboamu atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.’”
1 Wafalme 14:1-11 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Siku zile akaugua Abiya, mwana wa Yeroboamu. Yeroboamu akamwambia mkewe, Ondoka, tafadhali, ujibadilishe, wasikujue kuwa mkewe Yeroboamu; ukaende Shilo; tazama, yuko huko Ahiya nabii, aliyeninena mimi ya kwamba nitakuwa mfalme juu ya watu hawa. Twaa mkononi mikate kumi, na kaki, na mtungi wa asali, ukamwendee; naye atakuambia kijana atakuwaje. Akafanya hivi mkewe Yeroboamu, akaondoka, akaenda Shilo, akaja nyumbani kwa Ahiya. Basi Ahiya hakuweza kuona; kwa kuwa macho yake yamepofuka kwa sababu ya uzee wake. BWANA akamwambia Ahiya, Angalia, mkewe Yeroboamu anakuja akuulize mambo ya mwanawe; kwa maana ni mgonjwa; umwambie hivi na hivi; kwani itakuwa akiingia atajifanya kuwa mwanamke mwingine. Ikawa, Ahiya alipoisikia sauti ya miguu yake, akiingia mlangoni, alisema, Karibu, mkewe Yeroboamu; mbona wajifanya kuwa mwingine maana nimetumwa kwako wewe, mwenye maneno mazito. Nenda, umwambie Yeroboamu, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa nilikutukuza miongoni mwa watu, nikakufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli, nikaurarulia mbali ufalme utoke nyumba yake Daudi, na kukupa wewe; lakini wewe hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, aliyezishika amri zangu, na kunifuata kwa moyo wake wote, asifanye lolote ila yaliyo mema machoni pangu; lakini umekosa kuliko wote waliokutangulia, umekwenda kujifanyia miungu mingine, na sanamu zilizoyeyuka, unikasirishe, na kunitupa nyuma yako; tazama, kwa hiyo mimi nitaleta mabaya juu ya nyumba yake Yeroboamu, nami nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli, nami kuondoa nitawaondoa waliobaki wa nyumba yake Yeroboamu, kama mtu aondoavyo mavi, hata itakapokwisha pia. Yeye afaye wa Yeroboamu mjini mbwa watamla; afaye mashambani ndege wa angani watamla; kwa kuwa BWANA amelinena hilo.
1 Wafalme 14:1-11 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Siku zile akaugua Abiya, mwana wa Yeroboamu. Yeroboamu akamwambia mkewe, Ondoka, tafadhali, ujibadilishe, wasikujue kuwa mkewe Yeroboamu; ukaende Shilo; tazama, yuko huko Ahiya nabii, aliyeninena mimi ya kwamba nitakuwa mfalme juu ya watu hawa. Twaa mkononi mikate kumi, na kaki, na mtungi wa asali, ukamwendee; naye atakuambia kijana atakuwaje. Akafanya hivi mkewe Yeroboamu, akaondoka, akaenda Shilo, akaja nyumbani kwa Ahiya. Basi Ahiya hakuweza kuona; kwa kuwa macho yake yamepofuka kwa sababu ya uzee wake. BWANA akamwambia Ahiya, Angalia, mkewe Yeroboamu anakuja akuulize mambo ya mwanawe; kwa maana hawezi; hivi na hivi umwambie; kwani itakuwa akiingia atajifanya kuwa mwanamke mwingine. Ikawa, Ahiya alipoisikia sauti ya miguu yake, akiingia mlangoni, alisema, Karibu, mkewe Yeroboamu; mbona wajifanya kuwa mwingine maana nimetumwa kwako wewe, mwenye maneno mazito. Nenda, umwambie Yeroboamu, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa nilikutukuza miongoni mwa watu, nikakufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli, nikaurarulia mbali ufalme utoke nyumba yake Daudi, na kukupa wewe; walakini wewe hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, aliyezishika amri zangu, na kunifuata kwa moyo wake wote, asifanye lo lote ila yaliyo mema machoni pangu; lakini umekosa kuliko wote waliokutangulia, umekwenda kujifanyia miungu mingine, na sanamu zilizoyeyuka, unikasirishe, na kunitupa nyuma yako; tazama, kwa hiyo mimi nitaleta mabaya juu ya nyumba yake Yeroboamu, nami nitamkatia Yeroboamu kila mwanamume, aliyefungwa na aliyeachwa katika Israeli, nami kuondoa nitawaondoa waliobaki wa nyumba yake Yeroboamu, kama mtu aondoavyo mavi, hata itakapokwisha pia. Yeye afaye wa Yeroboamu mjini mbwa watamla; afaye mashambani ndege wa angani watamla; kwa kuwa BWANA amelinena hilo.
1 Wafalme 14:1-11 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Wakati ule, Abiya mwana wa Yeroboamu akaugua, naye Yeroboamu akamwambia mke wake, “Nenda ukajibadilishe, ili watu wasijue kwamba wewe ni mke wa Yeroboamu. Kisha uende Shilo. Nabii Ahiya, yule aliyeniambia kuwa nitakuwa mfalme wa watu hawa, yuko huko. Chukua mikate kumi, maandazi kadhaa na gudulia la asali na umwendee. Atakuambia kitakachotokea kwa kijana.” Basi mke wa Yeroboamu akafanya kama mumewe alivyosema, akaenda kwenye nyumba ya Ahiya huko Shilo. Wakati huu Ahiya alikuwa kipofu naye alishindwa kuona kwa sababu ya umri wake. Lakini Mwenyezi Mungu alikuwa amemwambia Ahiya, “Mke wa Yeroboamu anakuja kukuuliza kuhusu mwanawe, kwa kuwa ni mgonjwa, nawe utamjibu hivi na hivi. Atakapowasili, atajifanya kuwa ni mtu mwingine.” Hivyo, Ahiya aliposikia kishindo cha hatua zake mlangoni, akasema, “Karibu ndani, mke wa Yeroboamu. Kwa nini unajifanya kuwa si wewe? Nimetumwa kwako kukupa habari mbaya. Nenda, ukamwambie Yeroboamu kwamba hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Nilikuinua miongoni mwa watu na kukufanya mtawala wa watu wangu Israeli. Nikararua ufalme kutoka kwa nyumba ya Daudi na kukupa wewe, lakini hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, ambaye aliyashika maagizo yangu na kunifuata kwa moyo wake wote, akifanya tu lile lililokuwa sawa machoni pangu. Umefanya maovu mengi kuliko wote waliokutangulia. Umejitengenezea miungu mingine, sanamu za chuma, umenighadhibisha na kunigeuka. “ ‘Kwa sababu hii, nitaleta maafa juu ya nyumba ya Yeroboamu. Nitakatilia mbali kutoka kwa Yeroboamu kila mzaliwa wa mwisho wa kiume katika Israeli, mtumwa au mtu huru. Nitachoma nyumba ya Yeroboamu hadi iteketee yote kama mtu anavyochoma kinyesi. Mbwa watawala walio wa nyumba ya Yeroboamu watakaofia ndani ya mji, na ndege wa angani watawala wale watakaofia mashambani. Mwenyezi Mungu amenena!’