1 Wafalme 19:15-21
1 Wafalme 19:15-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Rudi kwa kupitia njia ya jangwani mpaka Damasko. Utakapofika, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu. Naye Yehu, mwana wa Nimshi, mpake mafuta awe mfalme wa Israeli. Elisha, mwana wa Shafati, wa Abel-mehola, utampaka mafuta awe nabii mahali pako. Basi, yeyote atakayenusurika upanga wa Hazaeli, Yehu atamuua, na yeyote atakayenusurika upanga wa Yehu, Elisha atamuua. Lakini, nitaacha hai watu 7,000 nchini Israeli, ambao hawajamwinamia Baali, wala kuibusu sanamu yake.” Elia akaondoka, akamkuta Elisha, mwana wa Shafati, analima. Hapo, palikuwa na jozi kumi na mbili za ng'ombe wanalima, na jozi ya Elisha ilikuwa ya nyuma kabisa. Basi, Elia akavua joho lake na kumtupia. Hapo, Elisha akawaacha ng'ombe wake, akamfuata Elia mbio na kumwambia, “Niruhusu kwanza niende kumpa baba yangu na mama yangu busu la kwaheri, kisha nikufuate.” Elia akamjibu, “Nenda! Kwani nimekuzuia?” Basi, Elisha akamwacha Elia, akairudia jozi yake ya ng'ombe, akawachinja ng'ombe hao na kuwapika akitumia miti ya nira kama kuni, akawapa watu, wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Elia na kuwa mtumishi wake.
1 Wafalme 19:15-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA akamwambia, Nenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako. Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua. Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu. Basi, akaondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng'ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake. Naye akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Nenda, urudi; ni nini niliyokutendea? Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng'ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng'ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia.
1 Wafalme 19:15-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako. Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua. Pamoja na hayo nitajisazia katika Israeli watu elfu saba, kila goti lisilomwinamia Baali, na kila kinywa kisichombusu. Basi, akaondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng’ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake. Naye akawaacha ng’ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Enenda, urudi; ni nini niliyokutendea? Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng’ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng’ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia.
1 Wafalme 19:15-21 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Mwenyezi Mungu akamwambia, “Rudi kwa njia uliyoijia, uende kwenye Jangwa la Dameski. Utakapofika huko, mpake Hazaeli mafuta awe mfalme wa Aramu. Pia mpake mafuta Yehu, mwana wa Nimshi awe mfalme wa Israeli, na umpake mafuta Al-Yasa mwana wa Shafati kutoka Abel-Mehola awe nabii baada yako. Yehu atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Hazaeli, naye Al-Yasa atamuua yeyote atakayeutoroka upanga wa Yehu. Hata sasa nimeweka akiba ya watu elfu saba katika Israeli, wote ambao hawajampigia Baali magoti, na wote ambao midomo yao haijambusu.” Hivyo Ilya akaondoka huko na kumkuta Al-Yasa mwana wa Shafati. Alikuwa akilima kwa jozi kumi na mbili za maksai, na yeye mwenyewe aliiongoza ile jozi ya kumi na mbili. Ilya akamwendea, na kumvisha vazi lake. Kisha Al-Yasa akawaacha maksai wake, akamkimbilia Ilya, akamwambia, “Niruhusu nikawabusu baba yangu na mama yangu, halafu nitafuatana nawe.” Ilya akajibu, “Rudi zako, kwani nimekufanya nini?” Basi Al-Yasa akamwacha Ilya, naye akarudi. Akachukua ile jozi yake ya maksai na kuwachinja. Akaipika ile nyama kwa kutumia miti ya nira kama kuni na kuwapa watu, nao wakala. Kisha akaondoka, akamfuata Ilya, akamtumikia.