1 Wafalme 2:36-46
1 Wafalme 2:36-46 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Tena, mfalme akatuma watu akamwita Shimei, akamwambia, Ujijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae ndani yake, wala usitoke humo kwenda mahali popote. Kwa kuwa siku ile ya kutoka kwako, na kuvuka kijito Kidroni, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe. Naye Shimei akamwambia mfalme, Neno hili ni jema; kama alivyosema bwana wangu mfalme, ndivyo atakavyofanya mtumwa wako. Basi Shimei akakaa Yerusalemu siku nyingi. Ikawa miaka mitatu ilipokwisha, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi, mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Wakamwambia Shimei, wakasema, Angalia, watumwa wako wako huko Gathi. Shimei akaondoka, akatandika punda wake, akaenda Gathi kwa Akishi, ili kuwatafuta watumwa wake. Akaenda Shimei, akawaleta watumwa wake toka Gathi. Naye Sulemani akaambiwa, ya kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu kwenda Gathi, na kurudi tena. Basi, mfalme akatuma watu, akamwita Shimei, akamwambia, Je! Sikukuapisha kwa BWANA, na kukushuhudia, kusema, Siku ile utakapotoka ukaenda mahali popote, ujue kwamba hakika utakufa? Nawe ukaniambia, Neno hili nililolisikia ni jema? Mbona basi hukukishika kiapo chako kwa BWANA, na amri niliyokuagiza? Tena, mfalme akamwambia Shimei, Umejua uovu wote uliouona moyoni mwako, uliomtenda Daudi baba yangu; basi kwa hiyo BWANA atakurudishia uovu wako kichwani pako mwenyewe. Ila mfalme Sulemani atakuwa amebarikiwa, na kiti cha enzi cha Daudi kitathibitika mbele za BWANA hata milele. Basi mfalme akamwamuru Benaya, mwana wa Yehoyada; naye akatoka, akampiga, hata akafa. Nao ufalme ukawa imara mkononi mwa Sulemani.
1 Wafalme 2:36-46 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Tena, mfalme akatuma watu akamwita Shimei, akamwambia, Ujijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae ndani yake, wala usitoke humo kwenda mahali po pote. Kwa kuwa siku ile ya kutoka kwako, na kuvuka kijito Kidroni, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe. Naye Shimei akamwambia mfalme, Neno hili ni jema; kama alivyosema bwana wangu mfalme, ndivyo atakavyofanya mtumwa wako. Basi Shimei akakaa Yerusalemu siku nyingi. Ikawa miaka mitatu ilipokwisha, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi, mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Wakamwambia Shimei, wakasema, Angalia, watumwa wako wako huko Gathi. Shimei akaondoka, akatandika punda wake, akaenda Gathi kwa Akishi, ili kuwatafuta watumwa wake. Akaenda Shimei, akawaleta watumwa wake toka Gathi. Naye Sulemani akaambiwa, ya kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu kwenda Gathi, na kurudi tena. Basi, mfalme akatuma watu, akamwita Shimei, akamwambia, Je! Sikukuapisha kwa BWANA, na kukushuhudia, kusema, Siku ile ya kutoka kwako ukienda mahali po pote, ujue hakika ya kwamba kufa utakufa? Nawe ukaniambia, Neno hili nililolisikia ni jema? Mbona basi hukukishika kiapo cha BWANA, na amri niliyokuagiza? Tena, mfalme akamwambia Shimei, Umejua uovu wote uliouona moyoni mwako, uliomtenda Daudi baba yangu; basi kwa hiyo BWANA atakurudishia uovu wako kichwani pako mwenyewe. Ila mfalme Sulemani atakuwa amebarikiwa, na kiti cha enzi cha Daudi kitathibitika mbele za BWANA hata milele. Basi mfalme akamwamuru Benaya, mwana wa Yehoyada; naye akatoka, akampiga, hata akafa. Nao ufalme ukawa imara mkononi mwa Sulemani.
1 Wafalme 2:36-46 Biblia Habari Njema (BHN)
Halafu mfalme akaagiza Shimei aitwe, akamwambia, “Jijengee nyumba humu Yerusalemu, ukae hapa bila kwenda mahali pengine popote pale. Maana siku utakapotoka na kuvuka kijito Kidroni, nakuambia kweli utakufa, na kujilaumu wewe mwenyewe kwa kifo chako.” Shimei akajibu, “Vema mfalme. Nitafanya kama ulivyosema.” Basi, akakaa Yerusalemu muda mrefu. Lakini mwishoni mwa mwaka wa tatu, watumwa wawili wa Shimei walitoroka, wakaenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi. Habari zilipomfikia kwamba wako Gathi, Shimei alipanda punda wake, akaenda huko kuwatafuta, kwa mfalme Akishi. Basi, akafika, akawapata, akawarudisha nyumbani. Mfalme Solomoni alipopata habari kwamba Shimei alikuwa ametoka Yerusalemu, akaenda Gathi na kurudi, alimwita Shimei na kumwambia, “Je, hukuniapia kwa jina la Mwenyezi-Mungu kwamba hutatoka Yerusalemu, nami sikukuonya kwa dhati kwamba, hakika utakufa kama utathubutu kwenda nje? Nawe ulikubali, ukaniambia, ‘Vema, nitatii.’ Mbona basi, umevunja kiapo chako kwa Mwenyezi-Mungu na kutojali amri niliyokupa?” Mfalme aliendelea kumwambia Shimei, “Unayajua wazi maovu uliyomtendea baba yangu Daudi, na sasa, kwa sababu ya hayo, Mwenyezi-Mungu atakuadhibu. Lakini mimi atanibariki, na kiti cha enzi cha Daudi kitaimarishwa mbele ya Mwenyezi-Mungu milele.” Hapo, mfalme akamwamuru Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka, akampiga na kumuua Shimei. Basi, ufalme ukaimarika chini ya Solomoni.
1 Wafalme 2:36-46 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kisha mfalme akatuma ujumbe kwa Shimei na kumwambia, “Ujijengee nyumba huko Yerusalemu uishi huko, lakini usiende mahali pengine popote. Siku utakayoondoka kuvuka Bonde la Kidroni, uwe na hakika utakufa; damu yako itakuwa juu ya kichwa chako mwenyewe.” Shimei akamjibu mfalme, “Ulilolisema ni jema. Mtumishi wako atatenda kama bwana wangu mfalme alivyosema.” Naye Shimei akakaa Yerusalemu kwa muda mrefu. Lakini baada ya miaka mitatu, watumwa wawili wa Shimei wakatoroka kwenda kwa Akishi mwana wa Maaka, mfalme wa Gathi, naye Shimei akaambiwa, “Watumwa wako wako Gathi.” Kwa ajili ya hili, Shimei akatandika punda wake, akaenda kwa Akishi huko Gathi kuwatafuta watumwa wake. Basi Shimei akaondoka na kuwarudisha watumwa wake kutoka Gathi. Solomoni alipoambiwa kuwa Shimei ametoka Yerusalemu na kwenda Gathi na amekwisha kurudi, mfalme akamwita Shimei na kumwambia, “Je, sikukuapiza kwa BWANA na kukuonya kuwa, ‘Siku utakayoondoka kwenda mahali pengine popote, uwe na hakika utakufa?’ Wakati ule uliniambia, ‘Ulilolisema ni jema. Nitatii!’ Kwa nini basi hukutunza kiapo chako kwa BWANA na kutii amri niliyokupa?” Pia mfalme akamwambia Shimei, “Unajua katika moyo wako makosa uliyomtendea baba yangu Daudi. Sasa BWANA atakulipiza kwa ajili ya mabaya yako uliyotenda. Lakini Mfalme Solomoni atabarikiwa, na kiti cha ufalme cha Daudi kitakuwa imara mbele za BWANA milele.” Kisha mfalme akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akatoka nje, akampiga Shimei na kumuua. Sasa ufalme ukawa umeimarika kikamilifu mikononi mwa Solomoni.