Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 22:29-40

1 Wafalme 22:29-40 Biblia Habari Njema (BHN)

Basi, mfalme wa Israeli akaenda pamoja na mfalme Yehoshafati wa Yuda, kuushambulia mji wa Ramoth-gileadi. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Mimi nitavaa mavazi yasiyo ya kifalme na kuingia vitani lakini wewe utavaa mavazi yako ya kifalme.” Hivyo mfalme wa Israeli akaenda vitani bila kuvaa mavazi ya kifalme. Mfalme wa Aramu alikuwa amewaamuru makapteni wake thelathini na wawili waliosimamia magari yake ya kukokotwa, akisema: “Msipigane na mtu yeyote yule, mkubwa au mdogo, ila tu na mfalme wa Israeli.” Baadaye, makapteni hao walipomwona Yehoshafati, walisema: “Kweli, huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo, walimwelekea, wakamshambulia; lakini Yehoshafati akapiga kelele. Makapteni walipotambua kwamba hakuwa mfalme wa Israeli waliacha kumshambulia, wakarudi. Lakini, askari mmoja wa Aramu, akauvuta upinde wake kwa kubahatisha, mshale ukamchoma mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma kifuani. Ahabu akamwambia dereva wa gari lake, “Geuza gari uniondoe vitani. Nimejeruhiwa!” Na mapigano siku hiyo yakazidi kuwa makali, huku mfalme ameegemeshwa garini, anawaelekea watu wa Aramu. Ilipofika jioni, akafariki. Damu ikawa inamtoka jerahani mwake na kutiririka hadi chini ya gari. Mnamo machweo ya jua, amri ikatolewa: “Kila mtu arudi mjini kwake; kila mtu arudi nchini kwake!” Mfalme Ahabu alipofariki maiti yake ilipelekwa Samaria, ikazikwa huko. Gari lake la kukokotwa waliliosha katika bwawa la Samaria, mbwa wakairamba damu yake, nao makahaba wakaoga humo, sawa kabisa na neno alilosema Mwenyezi-Mungu. Matendo mengine ya mfalme Ahabu, jinsi alivyojenga na kupamba nyumba yake kwa pembe, na miji yote aliyojenga, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli. Ahabu alipofariki, mwanawe Ahazia alitawala mahali pake.

1 Wafalme 22:29-40 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-Gileadi. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha, akaingia vitani. Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru wakuu wa magari yake thelathini na wawili, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake. Ikawa wakuu wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Huyo ndiye mfalme wa Israeli Wakageuka juu yake ili wapigane naye; naye Yehoshafati akapiga kelele. Ikawa, wakuu wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate. Mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana. Pigano likazidi siku ile; mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu ikatoka katika jeraha lake ndani ya gari. Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa, kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake. Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria. Wakaliosha gari penye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake; (basi ndipo walipooga makahaba); sawasawa na neno la BWANA alilolinena. Na mambo yote ya Ahabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na nyumba ya pembe aliyoijenga, na miji yote aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika Kitabu cha Kumbukumbu za Wafalme wa Israeli? Basi Ahabu akalala na baba zake; na Ahazia mwanawe akatawala mahali pake.

1 Wafalme 22:29-40 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani. Wakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na yeyote, mdogo au mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.” Wakati wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati akapiga kelele, wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli, nao wakaacha kumfuatilia. Lakini mtu fulani akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma. Mfalme akamwambia mwendesha gari lake, “Geuza gari na uniondoe mimi katika mapigano, nimejeruhiwa.” Vita vikaendelea mchana kutwa, naye Mfalme Ahabu akategemezwa ndani ya gari kuelekea Waaramu. Damu kutoka kwenye jeraha lake ikachuruzika ndani ya gari na jioni yake akafa. Jua lilipokuwa linazama, mbiu ikaenea katika jeshi lote: “Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake!” Basi mfalme akafa na akaletwa Samaria, nao wakamzika huko. Wakasafisha lile gari la vita katika bwawa la Samaria (mahali makahaba walipooga), na mbwa wakaramba damu yake, sawasawa na neno la BWANA lilivyokuwa limesema. Kwa matukio mengine ya utawala wa Ahabu, pamoja na yote aliyoyafanya, jumba la kifalme alilojenga na kupambwa kwa pembe za ndovu, nayo miji aliyoijengea maboma, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Israeli? Ahabu akalala pamoja na baba zake. Naye Ahazia mwanawe akawa mfalme baada yake.

1 Wafalme 22:29-40 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-Gileadi. Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha, akaingia vitani. Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru wakuu wa magari yake thelathini na wawili, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake. Ikawa wakuu wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Huyo ndiye mfalme wa Israeli Wakageuka juu yake ili wapigane naye; naye Yehoshafati akapiga ukelele. Ikawa, wakuu wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate. Mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana. Pigano likazidi siku ile; mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu ikatoka katika jeraha yake ndani ya gari. Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa, kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake. Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria. Wakaliosha gari penye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake; (basi ndipo walipooga makahaba); sawasawa na neno la BWANA alilolinena. Na mambo yote ya Ahabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na nyumba ya pembe aliyoijenga, na miji yote aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? Basi Ahabu akalala na baba zake; na Ahazia mwanawe akatawala mahali pake.