1 Wafalme 7:15-22
1 Wafalme 7:15-22 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana alizifanyiza zile nguzo mbili za shaba, mikono kumi na minane kwenda juu kwake kila moja; na uzi wa mikono kumi na miwili kuizunguka nguzo hii au hii. Akafanya taji mbili za shaba iliyoyeyushwa za kuwekwa juu ya vichwa vya nguzo; kwenda juu kwake taji moja mikono mitano, na mikono mitano kwenda juu kwake taji ya pili. Kulikuwa na nyavu kama kazi ya kusuka, na masongo ya mikufu, kwa taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; saba kwa taji moja, na saba kwa taji ya pili Hivyo akazifanya nguzo; na kulikuwa na safu mbili za kuzunguka juu ya wavu mmoja, zifunike taji zilizokuwako juu ya vichwa vya nguzo; akafanya vivyo hivyo kwa taji ya pili. Na taji zilizokuwa juu ya nguzo ukumbini zilikuwa za kazi ya mayungi, mikono minne. Kulikuwako tena taji juu ya nguzo mbili, karibu na uvimbe uliokuwako kando ya wavu; na makomamanga yalikuwa mia mbili, safu safu pande zote juu ya taji ya pili. Akazisimamisha nguzo ukumbini pa hekalu; akaisimamisha nguzo ya kuume, akaiita jina lake Yakini; akaisimamisha nguzo ya kushoto, akaiita jina lake Boazi. Na juu ya nguzo kulikuwa na kazi ya mayungi; hivyo mambo ya nguzo yakatimia.
1 Wafalme 7:15-22 Biblia Habari Njema (BHN)
Hiramu alitengeneza nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa mita 54, na mzingo wa mita 5.5. Ndani zilikuwa na tundu ambalo unene wa pande zake ulikuwa sentimita 2. Akatengeneza pia taji mbili za shaba, kila moja ikiwa na kimo cha mita 2.25; akaziweka juu ya nguzo hizo. Halafu, alifuma nyavu mbili zenye mapambo ya mrabamraba, akatengeneza na taji kwa kusokota mkufu: Vyote hivyo kwa ajili ya kupamba taji za shaba zilizowekwa juu ya zile nguzo. Hali kadhalika, alitengeneza matunda aina ya makomamanga, akayapanga safu mbili kuzunguka zile taji juu ya kila nguzo. Na taji hizo zilizokuwa juu ya nguzo mbele ya sebule, zilipambwa kwa mifano ya maua ya yungiyungi, kimo chake mita 1.75. Taji hizo zilikuwa juu ya hizo nguzo mbili, na pia zilikuwa juu ya sehemu ya mviringo iliyojitokeza karibu na zile nyavu. Palikuwa na mifano 400 ya matunda ya mkomamanga, imepangwa safu mbili kuzunguka kila taji. Hiramu aliziweka nguzo hizo kwenye sebule ya hekalu; nguzo aliyoisimika upande wa kusini iliitwa Yakini, na ile aliyoisimika upande wa kaskazini iliitwa Boazi. Vichwa vya nguzo hizo vilipambwa kwa mfano wa maua ya yungiyungi. Na hivyo kazi ya kutengeneza nguzo ikamalizika.
1 Wafalme 7:15-22 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana alizifanyiza zile nguzo mbili za shaba, mikono kumi na minane kwenda juu kwake kila moja; na uzi wa mikono kumi na miwili kuizunguka nguzo hii au hii. Akatengeneza mataji mawili ya shaba iliyoyeyushwa ya kuwekwa juu ya vichwa vya nguzo; kwenda juu kwake taji moja mikono mitano, na mikono mitano kwenda juu kwake taji la pili. Kulikuwa na nyavu kama kazi ya kusuka, na masongo ya mikufu, kwa mataji yaliyokuwako juu ya vichwa vya nguzo; saba kwa taji moja, na saba kwa taji la pili. Hivyo akazitengeneza nguzo; na kulikuwa na safu mbili za kuzunguka juu ya wavu mmoja, zifunike mataji yaliyokuwako juu ya vichwa vya nguzo; akafanya vivyo hivyo kwa taji la pili. Na mataji yaliyokuwa juu ya nguzo ukumbini yalikuwa ya kazi ya mayungi, mikono minne. Kulikuwako tena taji juu ya nguzo mbili, karibu na uvimbe uliokuwako kando ya wavu; na makomamanga yalikuwa mia mbili, safu safu pande zote juu ya taji la pili. Akazisimamisha nguzo ukumbini pa hekalu; akaisimamisha nguzo ya kulia, akaiita jina lake Yakini; akaisimamisha nguzo ya kushoto, akaiita jina lake Boazi. Na juu ya nguzo kulikuwa na kazi ya mayungi; hivyo mambo ya nguzo yakatimia.
1 Wafalme 7:15-22 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hiramu akasubu nguzo mbili za shaba, kila moja ikiwa na urefu wa dhiraa kumi na nane, kila nguzo ikiwa na mzingo wa dhiraa kumi na mbili kwa mstari. Pia alitengeneza mataji mawili ya shaba ya kusubu ili kuyaweka juu ya hizo nguzo; kila taji lilikuwa na kimo cha dhiraa tano kwenda juu. Wavu wa mikufu iliyosokotewa kwenye zile taji juu ya zile nguzo, saba kwa kila taji. Akatengeneza makomamanga katika safu mbili kuzunguka kila wavu kuremba mataji yaliyo juu ya nguzo. Alifanya hivyo kwa kila nguzo. Mataji yaliyokuwa juu ya nguzo kwenye baraza, yalikuwa katika umbo la yungiyungi, kimo chake ni dhiraa nne Juu ya mataji ya zile nguzo mbili, juu ya ile sehemu yenye umbo kama bakuli, karibu na ule wavu, kulikuwa na yale makomamanga 200 katika safu kuzunguka pande zote. Hiramu akasimamisha nguzo kwenye baraza ya Hekalu. Nguzo ya upande wa kusini akaiita Yakini, na ile ya upande wa kaskazini Boazi. Mataji yaliyokuwa juu yalikuwa na umbo la yungiyungi. Hivyo kazi ya nguzo ikakamilika.