Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 9:10-23

1 Wafalme 9:10-23 Biblia Habari Njema (BHN)

Kisha miaka ishirini ilipokwisha pita, ambayo Solomoni alizijenga zile nyumba mbili: Nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu, mfalme Solomoni alimpa Hiramu mfalme wa Tiro, miji ishirini katika mkoa wa Galilaya (kwa sababu huyo Hiramu alikuwa amempelekea Solomoni mbao za mierezi na miberoshi, na dhahabu pia, kadiri alivyohitaji kwa ujenzi). Lakini Hiramu alipowasili kutoka Tiro na kuiona miji hiyo aliyokuwa amepewa na Solomoni hakupendezwa nayo. Basi, akamwuliza Solomoni, “Ndugu yangu, ni miji gani hii ambayo umenipa?” Ndio sababu miji hiyo inaitwa nchi ya Kabuli hata leo. Hiramu alikuwa amempelekea mfalme Solomoni dhahabu kilo 3,600. Yafuatayo ni maelezo juu ya jinsi mfalme Solomoni alivyotumia kazi za kulazimishwa kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu yake, ngome ya Milo na ukuta wa Yerusalemu, na pia katika kujenga upya miji ya Hazori, Megido na Gezeri; (Gezeri ndio mji ambao Farao, mfalme wa Misri, alikuwa ameuteka, akauchoma moto na kuwaua Wakanaani, wakazi wake. Baadaye, binti Farao alipoolewa na Solomoni, mfalme wa Misri alimpa binti yake mji huo wa Gezeri uwe zawadi ya harusi. Basi, Solomoni aliujenga upya mji wa Gezeri); hali kadhalika alijenga Beth-horoni ya chini; kadhalika miji ifuatayo: Baalathi, na Tamari, mji ulio nyikani katika nchi ya Yuda na miji yake yote ya ghala, magari yake ya kukokotwa, na wapandafarasi wake; pia chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, Lebanoni au kwingineko katika ufalme wake. Watu wengine wote waliobaki miongoni mwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, yaani wote hao ambao hawakuwa wa taifa la Israeli, pamoja na wazawa wao ambao Waisraeli hawakuweza kuwaangamiza kabisa, Solomoni aliwafanyiza kazi za kulazimishwa hata leo. Lakini kati ya Waisraeli, Solomoni hakumfanya mtu yeyote kuwa mtumwa; wao ndio waliokuwa askari, watumishi wake, makamanda wake, maofisa wake, makamanda wa magari yake ya kukokotwa, na wapandafarasi wake. Ifuatayo ndiyo jumla ya maofisa wakuu waliohusika na uangalizi wa kazi ya Solomoni: Watu 550, hao ndio waliosimamia watu waliofanya kazi.

1 Wafalme 9:10-23 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alizijenga zile nyumba mbili, nyumba ya BWANA na nyumba yake mfalme, (basi Hiramu, mfalme wa Tiro, alikuwa amemletea Sulemani mierezi na miberoshi, na dhahabu, sawasawa na haja zake zote), ndipo mfalme Sulemani akampa Hiramu miji ishirini ya nchi ya Galilaya. Naye Hiramu akatoka Tiro kuitazama hiyo miji Sulemani aliyompa; wala hakupendezwa. Akasema, Miji gani hii uliyonipa, ndugu yangu? Akaiita nchi ya Kabuli, hata leo. Hiramu alikuwa amemletea mfalme talanta mia moja na ishirini za dhahabu. Na hii ndiyo sababu ya shokoa aliyoitoza mfalme Sulemani; ili kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba yake mwenyewe, na Milo, na ukuta wa Yerusalemu, na Hasori, na Megido, na Gezeri. Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda akautwaa Gezeri, na kuuteketeza kwa moto, akawaua Wakanaani waliokaa mjini, akampa zawadi binti yake, mkewe Sulemani. Naye Sulemani akaujenga Gezeri, na Beth-horoni wa chini, na Baalathi, na Tamari ulio nyikani, katika nchi; na miji yote ya hazina iliyokuwa yake Sulemani; na miji ya magari yake, na miji ya watu wake wapandao farasi, na kila alichopenda kujenga Sulemani huko Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake. Kwa habari ya watu wote waliosalia, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi, wasiokuwa wa wana wa Israeli; watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuweza kuwaharibu kabisa, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo. Lakini kwa wana wa Israeli Sulemani hakumtumikisha mtu yeyote shokoa; ila wao walikuwa askari, watumishi wake, makamanda wake, maafisa wake, makamanda wa magari yake na wapanda farasi wake. Hao maofisa wakuu, waliokuwa juu ya kazi yake Sulemani, walikuwa mia tano na hamsini, waliowasimamia watu watendao kazi.

1 Wafalme 9:10-23 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ikawa miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Sulemani alizijenga zile nyumba mbili, nyumba ya BWANA na nyumba yake mfalme, (basi Hiramu, mfalme wa Tiro, alikuwa amemletea Sulemani mierezi na miberoshi, na dhahabu, sawasawa na haja zake zote), ndipo mfalme Sulemani akampa Hiramu miji ishirini ya nchi ya Galilaya. Naye Hiramu akatoka Tiro kuitazama hiyo miji Sulemani aliyompa; wala haikumpendcza. Akasema, Miji gani hii uliyonipa, ndugu yangu? Akaiita nchi ya Kabuli, hata leo. Hiramu akamletea mfalme talanta sitini za dhahabu. Na hii ndiyo sababu ya shokoa aliyoitoza mfalme Sulemani; ili kuijenga nyumba ya BWANA, na nyumba yake mwenyewe, na Milo, na ukuta wa Yerusalemu, na Hazori, na Megido, na Gezeri. Farao, mfalme wa Misri, alikuwa amepanda akautwaa Gezeri, na kuuteketeza kwa moto, akawaua Wakanaani waliokaa mjini, akampa zawadi binti yake, mkewe Sulemani. Naye Sulemani akaujenga Gezeri, na Beth-horoni wa chini, na Baalathi, na Tamari ulio nyikani, katika nchi; na miji yote ya hazina iliyokuwa yake Sulemani; na miji ya magari yake, na miji ya watu wake wapandao farasi, na kila alichopenda kujenga Sulemani huko Yerusalemu, na katika Lebanoni, na katika nchi yote ya mamlaka yake. Kwa habari ya watu wote waliosalia, Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi, na Wayebusi, wasiokuwa wa wana wa Israeli; watoto wao waliosalia baada yao katika nchi, ambao wana wa Israeli hawakuweza kuwaharibu kabisa, katika hao Sulemani akawatumikisha shokoa hata leo. Lakini wa wana wa Israeli Sulemani hakumtumikisha mtu shokoa; ila ndio watu wa vita, na wangoje wake, na wakuu wake, na akida zake, na wakuu, wa magari yake, na wa wapanda farasi wake. Hao maakida wakuu, waliokuwa juu ya kazi yake Sulemani, walikuwa mia tano na hamsini, waliowaamuru watu watendao kazi.

1 Wafalme 9:10-23 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Miaka ishirini ilipopita, ambayo katika hiyo Solomoni alijenga majengo haya mawili, yaani Hekalu la BWANA na jumba la kifalme, Mfalme Solomoni akampa Hiramu mfalme wa Tiro miji ishirini katika Galilaya, kwa sababu Hiramu alikuwa amempatia mierezi yote, misunobari na dhahabu yote aliyohitaji. Lakini Hiramu alipotoka Tiro kwenda kuiona ile miji ambayo Solomoni alikuwa amempa, hakupendezwa nayo. Hiramu akauliza, “Hii ni miji ya namna gani uliyonipa, ndugu yangu?” Naye akaiita nchi ya Kabul, jina lililoko hadi leo. Basi Hiramu alikuwa amempelekea mfalme talanta 120 za dhahabu. Haya ni maelezo kuhusu kazi za kulazimishwa ambazo Mfalme Solomoni, alivyowafanyiza watu ili kulijenga hekalu la BWANA, na jumba lake la kifalme, na Milo, ukuta wa Yerusalemu, Hazori, Megido na Gezeri. (Farao mfalme wa Misri alikuwa ameushambulia na kuuteka mji wa Gezeri. Alikuwa ameuchoma moto. Akawaua Wakanaani waliokuwa wakikaa humo na kisha kuutoa kwa binti yake, yaani mkewe Solomoni, kama zawadi ya arusi. Solomoni akaujenga tena Gezeri.) Akajenga Beth-Horoni ya Chini, akajenga Baalathi na Tamari kwenye jangwa katika eneo la nchi yake, vilevile miji ya ghala na miji kwa ajili ya magari yake na kwa ajili ya farasi wake: chochote alichotaka kujenga katika Yerusalemu, katika Lebanoni, na katika eneo yote aliyotawala. Watu wote waliosalia kutoka kwa Waamori, Wahiti, Waperizi, Wahivi na Wayebusi (mataifa haya hayakuwa Waisraeli), yaani, wazao wao waliobakia katika nchi, ambao Waisraeli hawangeweza kuwaangamiza kabisa: hawa Solomoni akawalazimisha kuwa watumwa katika shokoa, kama ilivyo hadi leo. Lakini Solomoni hakumfanya yeyote wa Waisraeli kuwa mtumwa; wao ndio waliokuwa wapiganaji wake, maafisa wake wa serikali, maafisa wake, wakuu wake, majemadari wa jeshi wa magari yake ya vita na wapanda farasi. Pia walikuwa maafisa wakuu wasimamizi wa miradi ya Solomoni: maafisa 550 waliwasimamia watu waliofanya kazi.