1 Petro 1:10-12
1 Petro 1:10-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Manabii walipeleleza na kufanya uchunguzi juu ya wokovu huo, wakabashiri juu ya neema hiyo ambayo nyinyi mngepewa. Walijaribu kujua nyakati na mazingira ya tukio hilo, yaani wakati alioudokezea Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, akibashiri juu ya mateso yatakayompata Kristo na utukufu utakaofuata. Mungu aliwafunulia kwamba wakati walipokuwa wanasema juu ya hayo mambo ambayo nyinyi mmekwisha sikia sasa kutoka kwa wale wajumbe waliowatangazieni Habari Njema kwa nguvu ya Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni, hiyo kazi yao haikuwa kwa faida yao wenyewe, bali kwa ajili yenu. Hayo ndiyo mambo ambayo hata malaika wangependa kuyafahamu.
1 Petro 1:10-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kuhusu wokovu huo, manabii ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi, walichunguza sana. Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyaona.
1 Petro 1:10-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi. Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia.
1 Petro 1:10-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa, wakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alionyesha, alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata. Walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali waliwahudumia ninyi, waliponena kuhusu mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiria ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wanatamani kuyafahamu mambo haya.