1 Petro 4:1-6
1 Petro 4:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Maadamu Kristo aliteseka kimwili, nanyi pia mnapaswa kujiimarisha kwa nia hiyo yake; maana mtu akisha teseka kimwili hahusiki tena na dhambi. Tangu sasa, basi, maisha yaliyowabakia kuishi hapa duniani yanapaswa kuongozwa na matakwa ya Mungu, sio na tamaa za kibinadamu. Wakati uliopita mlikuwa na muda mrefu wa kufanya mambo wanayofanya watu wasiomjua Mungu. Mliishi maisha ya anasa, ubinafsi, ulevi, ugomvi, kunywa mno na ya ibada haramu za sanamu. Sasa, watu hao wasiomjua Mungu wanashangaa wanapoona kwamba hamwandamani nao tena katika hali ya kuishi vibaya, na hivyo wanawatukaneni. Lakini watapaswa kutoa hoja juu ya jambo hilo mbele yake Mungu aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa! Ndiyo maana Habari Njema ilihubiriwa hata kwa hao waliokufa, ili baada ya kuhukumiwa katika maisha yao ya kimwili kama wengine, waishi kwa ajili ya Mungu kwa njia ya Roho.
1 Petro 4:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Basi kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni silaha ya nia ile ile; kwa maana yeye aliyeteswa katika mwili ameachana na dhambi. Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani. Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuishi katika uzinzi, tamaa, ulevi, na karamu za kula na kunywa vileo kupindukia, na ibada haramu ya sanamu; mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana. Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa. Maana kwa ajili hiyo hata hao waliokufa walihubiriwa Injili, ili kwamba wahukumiwe katika mwili kama wahukumiwavyo wanadamu; bali wawe hai katika roho kama Mungu alivyo hai.
1 Petro 4:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Basi kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni silaha ya nia ile ile; kwa maana yeye aliyeteswa katika mwili ameachana na dhambi. Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani. Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali; mambo ambayo wao huona kuwa ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana. Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa. Maana kwa ajili hiyo hata hao waliokufa walihubiriwa Injili, ili kwamba wahukumiwe katika mwili kama wahukumiwavyo wanadamu; bali wawe hai katika roho kama Mungu alivyo hai.
1 Petro 4:1-6 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kwa hiyo, kwa kuwa Al-Masihi aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia hiyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi. Kwa hivyo, haishi maisha yake yaliyobaki hapa duniani ili kutimiza tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi ili kutimiza mapenzi ya Mungu. Kwa maana wakati uliopita, mmetumia muda mwingi mkifanya yale wapagani hupenda kutenda: wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya, na ibada chukizo za sanamu. Wao hushangaa kwamba ninyi hamjiingizi pamoja nao katika maisha yao ya uovu uliopita kiasi, nao huwatukana ninyi. Lakini itawapasa wao kutoa maelezo kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa. Kwa kuwa hii ndiyo sababu Injili ilihubiriwa hata kwa wale waliokufa, ili wahukumiwe sawasawa na wanadamu wengine katika mwili, lakini katika roho waishi kulingana na Mungu aishivyo.