1 Wathesalonike 1:4-10
1 Wathesalonike 1:4-10 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua muwe watu wake, maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi; tuliishi kwa manufaa yenu. Nyinyi mlifuata mfano wetu, mkamwiga Bwana. Ingawa mliteswa sana, mliupokea ujumbe huo kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu. Kwa hiyo nyinyi mmekuwa mfano mzuri kwa waamini wote wa Makedonia na Akaya. Maana, kutokana na bidii yenu ujumbe wa Bwana umesikika si huko Makedonia na Akaya tu, bali imani yenu kwa Mungu imeenea popote. Tena hatuhitaji kusema zaidi. Watu hao wanazungumza juu ya ziara yetu kwenu: Jinsi mlivyotukaribisha, jinsi mlivyoziacha sanamu, mkamgeukia Mungu aliye hai na wa kweli, na sasa mwamngojea Mwanae ashuke kutoka mbinguni, yaani Yesu, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu na ambaye anatuokoa katika ghadhabu ya Mungu inayokuja.
1 Wathesalonike 1:4-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, tunajua uteule wenu; ya kwamba Injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu. Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu. Hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya. Maana kutoka kwenu neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea; hata hatuna haja sisi kunena lolote. Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli; na kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa kutoka kwa ghadhabu itakayokuja.
1 Wathesalonike 1:4-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Kwa maana, ndugu mnaopendwa na Mungu, twajua uteule wenu; ya kwamba injili yetu haikuwafikia katika maneno tu, bali na katika nguvu, na katika Roho Mtakatifu, na uthibitifu mwingi; kama vile mnavyojua jinsi zilivyokuwa tabia zetu kwenu, kwa ajili yenu. Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya Roho Mtakatifu. Hata mkawa kielelezo kwa watu wote waaminio katika Makedonia, na katika Akaya. Maana kutoka kwenu neno la Mungu limevuma, si katika Makedonia na Akaya tu, ila na kila mahali imani yenu mliyo nayo kwa Mungu imeenea; hata hatuna haja sisi kunena lo lote. Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli; na kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu, mwenye kutuokoa na ghadhabu itakayokuja.
1 Wathesalonike 1:4-10 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Ndugu zetu mnaopendwa na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua, kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho wa Mungu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda kati yenu kwa ajili yenu. Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana Isa, ingawa mlipata mateso mengi, mlilipokea lile Neno kwa furaha katika Roho wa Mungu. Hivyo ninyi mkawa kielelezo kwa waumini wote katika Makedonia na Akaya. Kwa maana kutoka kwenu neno la Bwana Isa limesikika, si katika Makedonia na Akaya tu, bali pia imani yenu katika Mungu imejulikana kila mahali, kiasi kwamba hatuna haja ya kusema chochote juu yake. Kwa maana watu wa maeneo hayo wenyewe wanaeleza jinsi mlivyotupokea na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli, na ili kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu: yaani Isa, yeye aliyetuokoa kutoka ghadhabu inayokuja.