1 Wathesalonike 2:5-12
1 Wathesalonike 2:5-12 Biblia Habari Njema (BHN)
Maana kama mjuavyo, sisi hatukutumia maneno ya kubembeleza wala hatukutumia maneno ya kijanja ya kuficha ubinafsi fulani; Mungu ni shahidi! Hatukutafuta sifa kutoka kwa watu, wala kutoka kwenu, wala kutoka kwa mtu yeyote, ingawa sisi tukiwa mitume wa Kristo, tungeweza kudai mambo fulani kwenu. Lakini sisi tulikuwa wapole kati yenu kama alivyo mama kwa watoto wake. Tuliwapenda nyinyi sana hata tukawa tayari kuwashirikisha si tu Habari Njema ya Mungu, bali pia na maisha yetu. Ndivyo mlivyokuwa wapenzi wetu! Ndugu, nyinyi mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi na kutaabika. Tulipowaleteeni Habari Njema ya Mungu tulifanya kazi mchana na usiku kusudi tusiwe mzigo kwa mtu yeyote miongoni mwenu. Nyinyi mnaweza kushuhudia, na Mungu pia ni shahidi, kwamba mwenendo wetu kati yenu nyinyi mnaoamini ulikuwa mzuri, mwadilifu na bila lawama. Mnajua kwamba sisi tulimtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea watoto wake mwenyewe. Tuliwatia moyo, tuliwafariji na kuwahimiza ili mpate kuishi maisha yampendezayo Mungu ambaye anawaiteni mshiriki ufalme na utukufu wake.
1 Wathesalonike 2:5-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wowote, kama mjuavyo, wala maneno ya juu juu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi. Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine, ingawa tungeweza kuwalemea kama Mitume wa Kristo; bali tulikuwa wapole katikati yenu, kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe. Hivyo ndivyo nasi tukiwajali kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu. Maana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, huku tukiwahubiria Injili ya Mungu. Ninyi ni mashahidi, na Mungu pia, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa; vile vile, kama mjuavyo, jinsi tulivyomwonya kila mmoja wenu kama baba awaonyavyo watoto wake mwenyewe, tukiwatia moyo na kushuhudia; ili mwende kama ilivyo wajibu wenu kwa Mungu, mwenye kuwaita ninyi ili mwingie katika ufalme wake na utukufu wake.
1 Wathesalonike 2:5-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Maana hatukuwa na maneno ya kujipendekeza wakati wo wote, kama mjuavyo, wala maneno ya juujuu ya kuficha choyo; Mungu ni shahidi. Hatukutafuta utukufu kwa wanadamu, wala kwenu, wala kwa wengine tulipokuwa tukiweza kuwalemea kama mitume wa Kristo; bali tulikuwa wapole katikati yenu, kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe. Vivyo hivyo nasi tukiwatumaini kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu. Maana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu. Ninyi ni mashahidi, na Mungu pia, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa; vile vile, kama mjuavyo, jinsi tulivyomwonya kila mmoja wenu kama baba awaonyavyo watoto wake mwenyewe, tukiwatia moyo na kushuhudia; ili mwenende kama ilivyo wajibu wenu kwa Mungu, mwenye kuwaita ninyi ili mwingie katika ufalme wake na utukufu wake.
1 Wathesalonike 2:5-12 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Kama mnavyojua, hatukuja kwenu kwa maneno ya kujipendekeza au maneno yasiyo ya kweli ili kuficha tamaa mbaya; Mungu ndiye shahidi yetu. Hatukuwa tukitafuta sifa kutoka kwa wanadamu, wala kutoka kwenu au kwa mtu mwingine yeyote, ingawa kama mitume wa Al-Masihi tungeweza kuwa mzigo kwenu. Lakini tulikuwa wapole kati yenu, kama vile mama anawatunza watoto wake wadogo. Tuliwapenda sana, kiasi kwamba tulifurahia kushirikiana nanyi, si Injili ya Mungu tu, bali hata maisha yetu, kwa sababu mlikuwa wa thamani mno kwetu. Ndugu zetu, mnakumbuka juhudi yetu na taabu yetu. Tulifanya kazi usiku na mchana, ili tusiwe mzigo kwa mtu yeyote tulipokuwa tukiwahubiria Injili ya Mungu. Ninyi wenyewe ni mashahidi na Mungu pia, jinsi tulivyokuwa watakatifu, wenye haki na wasio na lawama miongoni mwenu ninyi mlioamini. Maana mnajua kwamba tuliwatendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea watoto wake. Tuliwatia moyo, tukiwafariji na kuwahimiza kuishi maisha yanayompendeza Mungu, anayewaita katika ufalme wake na utukufu wake.