1 Timotheo 1:1-7
1 Timotheo 1:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)
Mimi Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo tumaini letu, nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu. Napenda ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao. Waambie waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani. Shabaha ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na imani ya kweli. Watu wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana. Wanapenda kuwa waalimu wa sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo wanayosisitiza.
1 Timotheo 1:1-7 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, tarajio letu; kwa Timotheo, mwanangu halisi katika imani. Na iwe kwako neema, rehema na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Kama vile nilivyokusihi ukae Efeso, nilipokuwa nikisafiri kwenda Makedonia, ili uwakataze wengine wasifundishe elimu nyingine; wala wasiangalie hadithi na nasaba zisizo na kikomo, zinazozua maswali wala si mpango wa Mungu ulio katika imani; basi uwaambie hivyo. Lakini lengo la agizo hili ni kuleta upendo utokao katika moyo safi na dhamiri njema, na imani isiyo na unafiki. Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili; wakitaka kuwa waalimu wa sheria, ingawa hawayafahamu wasemayo wala mambo yale wayanenayo kwa uthabiti.
1 Timotheo 1:1-7 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Paulo, mtume wa Kristo Yesu, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Kristo Yesu, taraja letu; kwa Timotheo, mwanangu hasa katika imani. Neema na iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu. Kama vile nilivyokusihi ukae Efeso, nilipokuwa nikisafiri kwenda Makedonia, ili uwakataze wengine wasifundishe elimu nyingine; wala wasiangalie hadithi na nasaba zisizo na ukomo, ziletazo maswali wala si madaraka ya Mungu yaliyo katika imani; basi ufanye hivyo. Walakini mwisho wa agizo hilo ni upendo utokao katika moyo safi na dhamiri njema, na imani isiyo na unafiki. Wengine wakiyakosa hayo wamegeukia maneno ya ubatili; wapenda kuwa waalimu wa sheria, ingawa hawayafahamu wasemayo wala mambo yale wayanenayo kwa uthabiti.
1 Timotheo 1:1-7 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu, na ya Al-Masihi Isa aliye tumaini letu. Kwa Timotheo, mwanangu halisi katika imani. Neema, rehema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba Mwenyezi na kwa Al-Masihi Isa, Bwana wetu. Kama nilivyokusihi wakati nilipoenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani. Kusudi la maagizo haya ni upendo unaotoka katika moyo safi, dhamiri safi na imani ya kweli. Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, wanataka kuwa walimu wa Torati, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.