Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Timotheo 3:1-16

1 Timotheo 3:1-16 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Hili ni neno la kuaminiwa, kwamba mtu akitamani kazi ya uangalizi, atamani kazi nzuri. Basi, imempasa mwangalizi awe mtu asiye na lawama, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi, anayejitawala, anayeheshimika, mkarimu, ajuaye kufundisha, asiwe mlevi, wala mkali bali awe mpole, asiwe mgomvi wala mpenda fedha. Lazima aweze kuisimamia nyumba yake mwenyewe vizuri na kuhakikisha kwamba watoto wake wanamtii na kuwa na heshima kwa kila njia. (Kwa maana kama mtu hajui jinsi ya kusimamia nyumba yake mwenyewe, atawezaje kuliangalia kanisa la Mungu?) Asiwe mtu aliyeokoka karibuni asije akajivuna na kuangukia kwenye hukumu ile ile ya ibilisi. Inampasa pia awe na sifa njema kwa watu walio nje, ili asije akalaumiwa na kuanguka kwenye mtego wa ibilisi. Vivyo hivyo, mashemasi nao wawe watu wanaostahili heshima, wasiwe wenye kauli mbili au wenye kujifurahisha kwa mvinyo, wala wanaotamani faida isiyo halali. Inawapasa kushikamana sana na ile siri ya imani kwa dhamiri safi. Ni lazima wapimwe kwanza; kisha kama hakuna neno dhidi yao, basi na waruhusiwe kuhudumu kama mashemasi. Vivyo hivyo, wake zao wawe wanawake wanaostahili heshima, wasio wasingiziaji, bali wawe na kiasi na waaminifu katika kila jambo. Shemasi awe mume wa mke mmoja na inampasa aweze kusimamia watoto wake na watu wa nyumbani mwake vyema. Wale ambao wamehudumu vyema katika huduma ya ushemasi hujipatia msimamo bora na ujasiri mkubwa katika imani yao ndani ya Kristo Yesu. Ingawa ninatarajia kuja kwako hivi karibuni, ninakuandikia maagizo haya sasa ili kwamba, kama nikikawia, utajua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, ambayo ndiyo kanisa la Mungu aliye hai, lililo nguzo na msingi wa kweli. Bila shaka yoyote, siri ya utauwa ni kubwa: Alidhihirishwa katika mwili wa kibinadamu, akathibitishwa kuwa na haki katika Roho, akaonekana na malaika, akahubiriwa miongoni mwa mataifa, akaaminiwa ulimwenguni, akachukuliwa juu katika utukufu.

1 Timotheo 3:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

Msemo huu ni wa kweli: Mtu anayetaka kuwa askofu, huyo anatamani kazi nzuri. Basi, askofu anapaswa kuwa mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu; ni lazima awe mkarimu na anayeweza kufundisha; asiwe mlevi au mtu wa matata, bali awe mpole, apendaye amani; asiwe mtu wa kupenda fedha; anapaswa awe mtu awezaye kuongoza vema nyumba yake, na kuwafanya watoto wake wawe watii kwa heshima yote. Maana kama mtu hawezi kuongoza vema nyumba yake, atawezaje kulitunza kanisa la Mungu? Mtu ambaye hajakomaa bado katika imani asifanywe kuwa kiongozi katika kanisa, asije akajaa majivuno na kuhukumiwa kama vile Ibilisi alivyohukumiwa. Anapaswa awe mwenye sifa njema kati ya watu walio nje ya kanisa, ili asije akalaumiwa na kuanguka katika mtego wa Ibilisi. Wasaidizi katika kanisa wanapaswa pia kuwa watu wenye tabia njema na wanyofu; wasiwe wanywaji mno wa divai au wenye tamaa ya fedha; wanapaswa kuzingatia kwa dhamiri njema ukweli wa ndani wa imani. Ni lazima kwanza wathibitishwe, na wakionekana kuwa wanafaa, basi, watoe huduma yao. Wake zao wanapaswa pia kuwa na tabia njema, wasiowasengenya watu, wenye kiasi na waaminifu katika mambo yote. Msaidizi katika kanisa lazima awe na mke moja tu, na awezaye kuongoza vema watoto wake na nyumba yake. Maana wasaidizi wanaofanya kazi yao vizuri hujipatia msimamo mzuri, na wanaweza kusema bila hofu juu ya imani yao katika Kristo Yesu. Ninakuandikia barua hii nikiwa na matumaini ya kuja kwako hivi karibuni. Lakini kama nikicheleweshwa, basi, barua hii itakufahamisha mwenendo tunaopaswa kuwa nao katika nyumba ya Mungu, ambayo ni kanisa la Mungu aliye hai, na ambalo ni nguzo na msingi wa ukweli. Hakuna mashaka yoyote juu ya ukuu wa siri ya dini yetu: Alionekana katika umbo la kibinadamu, alithibitishwa na Roho kuwa ni mwadilifu, akaonekana na malaika. Alihubiriwa kati ya mataifa, aliaminiwa ulimwenguni, akachukuliwa juu katika utukufu.

1 Timotheo 3:1-16 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkarimu, ajuaye kufundisha; asiwe mtu wa kulewa, asiye dhalimu; bali awe mpole; asiwe mbishi, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi. Vivyo hivyo mashemasi na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana, si watu wanaotamani fedha ya aibu; wakiishika siri ya imani kwa dhamiri safi. Hawa pia na wajaribiwe kwanza; baadaye waitende kazi ya shemasi, wakiisha kuonekana kuwa hawana hatia. Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; wasiwe wachongezi; ila wawe watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote. Mashemasi na wawe waume wa mke mmoja, wakiwasimamia watoto wao vizuri, na nyumba zao. Kwa maana watendao vema kazi ya shemasi hujipatia daraja nzuri, na ujasiri mwingi katika imani iliyo katika Kristo Yesu. Nakuandikia hayo nikitaraji kuja kwako hivi karibu. Lakini nikikawia, upate kujua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, iliyo kanisa la Mungu aliye hai, nguzo na msingi wa kweli. Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulikana kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.

1 Timotheo 3:1-16 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema. Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha; si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha; mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu; (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi. Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi. Vivyo hivyo mashemasi8 na wawe wastahivu; si wenye kauli mbili, si watu wa kutumia mvinyo sana, si watu wanaotamani fedha ya aibu; wakiishika siri ya imani katika dhamiri safi. Hawa pia na wajaribiwe kwanza; baadaye waitende kazi ya shemasi, wakiisha kuonekana kuwa hawana hatia. Vivyo hivyo wake zao na wawe wastahivu; si wasingiziaji; watu wa kiasi, waaminifu katika mambo yote. Mashemasi na wawe waume wa mke mmoja, wakiwasimamia watoto wao vizuri, na nyumba zao. Kwa maana watendao vema kazi ya shemasi hujipatia daraja nzuri, na ujasiri mwingi katika imani iliyo katika Kristo Yesu. Nakuandikia hayo nikitaraji kuja kwako hivi karibu. Lakini nikikawia, upate kujua jinsi iwapasavyo watu kuenenda katika nyumba ya Mungu, iliyo kanisa la Mungu aliye hai, nguzo na msingi wa kweli. Na bila shaka siri ya utauwa ni kuu. Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho, Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu katika utukufu.