1 Timotheo 5:1-8
1 Timotheo 5:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Usimkemee mwanamume mzee, bali msihi kama vile angekuwa baba yako. Watendee vijana wa kiume kama ndugu zako, wanawake wazee kama mama zako, na vijana wa kike kama dada zako, kwa usafi wote. Waheshimu wanawake wajane walio wajane kweli. Lakini mjane aliye na watoto au wajukuu, hao wanapaswa kujifunza kutimiza wajibu wao wa kidini kwa jamaa zao wenyewe na hivyo kuwalipa wazazi wao na wazee wao, kwani hilo ni jambo la kupendeza mbele ya Mungu. Mwanamke mjane kweli, asiye na mtu wa kumsaidia, amemwekea Mungu tumaini lake na huendelea kusali na kumwomba msaada usiku na mchana. Lakini mwanamke ambaye huishi maisha ya anasa, huyo amekufa, ingawa yu hai. Wape maagizo haya, wasije wakawa na lawama. Lakini kama mtu hawatunzi watu wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani kwake, basi, mtu huyo ameikana imani, na ni mbaya zaidi kuliko mtu asiyeamini.
1 Timotheo 5:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na wanaume vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku. Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai. Mambo hayo pia uyaagize, ili wasiwe na lawama. Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.
1 Timotheo 5:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mzee usimkemee, bali umwonye kama baba; na vijana kama ndugu; wanawake wazee kama mama; wanawake vijana kama ndugu wa kike; katika usafi wote. Uwaheshimu wajane walio wajane kweli kweli. Lakini mjane akiwa ana watoto au wajukuu, na wajifunze kwanza kuyatenda yaliyo wajibu wao kwa jamaa zao wenyewe, na kuwalipa wazazi wao. Kwa kuwa hili lakubalika mbele za Mungu. Basi yeye aliye mjane kweli kweli, ameachwa peke yake, huyo amemwekea Mungu tumaini lake, naye hudumu katika maombi na sala mchana na usiku. Bali, yeye asiyejizuia nafsi yake amekufa ingawa yu hai. Mambo hayo pia uyaagize, ili wasiwe na lawama. Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.
1 Timotheo 5:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Usimkemee mzee kwa ukali bali umshawishi kama vile angekuwa ni baba yako. Uwatendee vijana kama vile ndugu zako; nao wanawake wazee uwatendee kama mama zako, na wanawake vijana kama dada zako, katika usafi wote. Waheshimu wanawake wajane ambao ni wajane kweli kweli. Kama mjane ana watoto ama wajukuu, hawa inawapasa awali ya yote wajifunze kutimiza wajibu wao wa kumcha Mungu katika matendo kwa kuwatunza wale wa jamaa zao wenyewe, na hivyo wawarudishie wema waliowatendea wazazi wao, kwa kuwa hivi ndivyo impendezavyo Mungu. Mwanamke ambaye ni mjane kweli kweli, yaani, yeye aliyebaki peke yake huweka tumaini lake kwa Mungu naye hudumu katika maombi usiku na mchana akimwomba Mungu ili amsaidie. Lakini mjane aishiye kwa anasa amekufa, ingawa anaishi. Wape watu maagizo haya pia, ili asiwepo yeyote wa kulaumiwa. Kama mtu hawatunzi wale wa jamaa yake, hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko yeye asiyeamini.